Huu ni wakati mwingine ambao Bwana amenijalia kuwepo kwa kusudi lake jema. Nitaelezea katika somo hili kuhusu dhambi ilivyo na madhara kwa mtu aitendaye. Kwanza tuangalie dhambi ilivyoanza kwa Adamu na Hawa ni wakati walipokula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya ambayo Mungu aliwakataza wasile. Kwa sababu hiyo dhambi ilisababisha madhara mengi kwa uzao wake na vizazi vyote duniani. Kwa hiyo shida zote zilizopo duniani zimetokana na dhambi.
Kutokana na wazazi wetu wa kwanza Adamu na Hawa kwa kuwa walitenda dhambi na vizazi vingine vyote vimehesabiwa ni wenye dhambi. Mtu anazaliwa akiwa na asili ya dhambi kutoka kwa wazazi wa kwanza Adamu na Hawa. Warumi 3:23
“kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;”
Kutokana na sababu hiyo ndio maana kila mwanadamu anakufa sawasawa na Mungu alivyosema katika kitabu cha Mwanzo 2:16-17 “BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.”
Sasa unaweza kuona ulimwenguni kote shida na dhiki zote zilizopo ni kwa sababu ya dhambi ya mwanadamu. Kwa sababu hiyo dhambi imesababisha vita, njaa, magonjwa, kifo, wivu, hasira, chuki, mafarakano, mvua kuzuiwa kunyesha, nakadhalika. Hayo yote yasingekuwepo kama mwanadamu asingelitenda dhambi. Kwa hiyo unaweza kuona Dhambi ilivyo mbaya, na madhara yake ni mengi.
Kinachotokea kwa mtu atendaye dhambi. Mkristo ambaye ameokoka na kuishi katika neno la Mungu na utakatifu, na baadae kuamua kuishi katika dhambi kinachotokea katika maisha yake ni kama ifuatavyo;
1.Anapoteza uhusiano wake na Mungu, pia anakuwa ametengana na Mungu. Akiomba maombi yake hayatasikilizwa. Isaya 59:2
“lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.” Mithali 15:29 “BWANA yu mbali na wasio haki; Bali huisikia sala ya mwenye haki.”
2.Jina lake linafutwa kwenye kitabu cha uzima wa milele. Kutoka 32:33
“BWANA akamwambia Musa, Mtu ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu.”
3. Mema yote aliyoyatenda hayatakumbukwa. Ezekieli 18:24
“Bali mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, na kufanya machukizo yote kama yale afanyayo mtu mwovu, je, ataishi? Katika matendo yake yote ya haki aliyoyatenda halitakumbukwa hata mojawapo. Katika kosa lile alilolikosa, naam, katika dhambi yake aliyoitenda, atakufa.”
4. Anapoteza amani na furaha ya Mungu katika maisha yake. Kwa sababu hiyo hatakuwa na amani wala furaha. Isaya 57:20-21 “Bali wabaya wanafanana na bahari iliyochafuka; maana haiwezi kutulia, na maji yake hutoa tope na takataka. Hapana amani kwa wabaya; asema Mungu wangu.”
5. Anakuwa upande wa Shetani. 1 Yohana 3:8 “atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo…”
6. Anakuwa amekataliwa na Mungu na katika kanisa. Kwa sababu hiyo hana sehemu ya ushirika na watakatifu. Ndio maana imeandikwa, 1 Wakorintho 5:12-13 “... Ninyi mwondoeni yule mbaya miongoni mwenu.”
7. Roho yake inakuwa imekufa. Ndani yake hana uzima wa milele, wala amani. Warumi 6:23
“Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Ezekieli 18:20 “Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake.” Warumi 8:6 “Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani.” Kwa sababu hiyo mtu atendaye dhambi roho yake inapokufa na mwili nao utakufa. Mithali 10:7 “Kumcha BWANA kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa.”
8. Anakuwa amepoteza hofu ya Mungu. Wala hamwogopi Mungu katika maisha yake. Zaburi 36:1
“Kuasi kwake yule mwovu hunena moyoni mwake, Hakuna hofu ya Mungu mbele ya macho yake.” Luka 12:5 “Lakini nitawaonya mtakayemwogopa; mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo.”
9. Kuhukumiwa na kutupwa katika moto wa milele. Mathayo 18:8 “Basi mkono wako au mguu wako ukikukosesha, ukate ukautupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima hali umepungukiwa na mkono au mguu, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili, na kutupwa katika moto wa milele.” Ufunuo wa Yohana 14:11
“Na moshi wa maumivu yao hupanda juu hata milele na milele, wala hawana raha mchana wala usiku, hao wamsujuduo huyo mnyama na sanamu yake, na kila aipokeaye chapa ya jina lake.”
10 Anakuwa ni adui wa Mungu kutokana na maisha ya dhambi. Mtu aishiye katika dhambi kwake ni jambo gumu kuitii sheria ya Mungu na kumpendeza. Warumi 8:6-8 “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu.”
11. Anakuwa amekataliwa na Mungu na katika kanisa. Kwa sababu hiyo hana sehemu ya ushirika na watakatifu. Ndio maana imeandikwa, 1 Wakorintho 5:12-13 “... Ninyi mwondoeni yule mbaya miongoni mwenu.”
Wampendao Mungu na neno lake.
Kwa upande mwingine ni muhimu kuwa makini kwa sababu kuna baadhi ya wakristo ambao wanafanya makosa bila kujua au kukusudia. Lakini katika maisha yao wanampenda Mungu na neno lake. Wakristo wa namna hiyo wanapotambua makosa yao ni rahisi kumngeukia Mungu na kutubu. Wagalatia 6:1-2 “Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.” Mathayo 18:15-17 “Na ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye, wewe na yeye peke yenu; akikusikia, umempata nduguyo. La, kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike. Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru;
imekaaa vizuri sana
JibuFutaBarikiwa mtumishi kwa ujumbe nzuri unaobariki
JibuFuta
JibuFutawow! Barikiwa sana Mtumishi wa MUNGU kazi yako ni njema sana machoni pa Bwana.
Asante mtumishi kwa neno la Uponyaji
JibuFutaMungu akubariki Sana Na akutendee mema
JibuFutaUbarikiwe sana mtumishi wa Bwana
JibuFutaIko SAWA barikiwa sana
JibuFutaMungu akubariki mutumishi
JibuFuta