Ninajua Mungu aliumba ulimwengu na vyote vilivyomo na vinatokana na yeye. Na pia aliweka majira na wakati, tunaweza kufahamu na kuona kuna majira ya mchana na usiku. Yote hayo aliyafanya kwa kusudi lake kamili. Tukiangalia kusudi la Mungu kumuumba mwanadamu ni ili amtumikie na kumwabudu.
Kwa sababu hiyo yampasa mkristo aliyeokoka au mtumishi wa Mungu kuukomboa wakati na kuutumia muda kila siku kwa ajili ya kuutafuta uso wa Mungu. Ni muhimu kufahamu ya kwamba muda ukishapita kama hujautumia vizuri hautarudi tena.Ukishaupoteza muda unakuwa umepata hasara. Ijapokuwa mtu anaweza kuwa na shughuli nyingi za kila siku katika maisha yake ni muhimu atenge muda kwa ajili kufanya ibada mbele za Mungu. Angalao atenge muda wa lisaa limoja asubuhi na jioni lisaa limoja. Yesu alipokuwa na wale wanafunzi wake Katika maombi kwenye bustani ya Gethsemane alifikiri wangeomba hata lisaa limoja. “Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa? Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu”. Mathayo 26:40.
Jambo lingine la kuangalia ni muhimu kuepuka mambo ambayo sii ya lazima. Jihadhari na kuwa na kiasi usitumie muda wako mwingi zaidi kwenye Facebook, TV, Whatsapp, Twitter, na biashara. Mambo hayo huchukua nafasi na kukupotozea muda wa kumtafuta Mungu. Kama utautumia muda vizuri utakuwa na muda mwingi zaidi wa kuutafuta uso wa Mungu. Mkristo aliye na bidii ya kuutafuta uso wa Mungu na kumpendeza anakuwa na amani itokayo kwa Mungu. Pia anakuwa karibu sana na Mungu. Naye Roho Mtakatifu atampasha habari kutoka kwa Mungu. “...huyo Roho wa kweli... hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari”. Yohana 16:13-14. Kusoma zaidi bofya hapa; Mungu anavyosema.
Tuaweza kujifunza kutoka kwa Yesu ya kwamba alikuwa na ratiba ambayo ilikuwa ya kudumu kwa ajili ya kuutafuta uso wa Mungu. “Basi, kila mchana alikuwa akifundisha hekaluni, na usiku huenda kulala katika mlima uitwao wa Mizeituni. Akatoka akaenda mpaka mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake nao wakafuatana naye”. Luka 21:37; 22:39. Haya maandiko yanaonesha wazi ya kwamba ilikuwa ni desturi kwake kwenda mlimani kuomba kila siku. Kwa sababu hiyo ndio maana alikuwa na uwezo na mamlaka ya Mungu juu yake. Hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kumshinda yule maovu na majaribu yake na kuwa salama kama hafanyi maombi kila siku. Ndio maana mstari wa hapo juu Yesu alisema ‘ombeni msije mkaingia majaribuni.’
Alitahadharisha kwa kusema maneno hayo kwa sababu shetani siku zote anawatafuta wale ambao wamesimama imara katika Mungu ili kuwajaribu wamkosee Mungu. Ndio maana alimjaribu Yesu na Mitume nao wakamshinda kwa maombi na neno la Mungu. Kulifamu neno la Mungu ni muhimu ili tuweze kugundua uongo wa Shetani na kumpinga. “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze”. 1 Petro 5:8. “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.
Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili”. Yakobo 4:7-8.
Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili”. Yakobo 4:7-8.
Maoni
Chapisha Maoni