Maana ya neno sabato.
Sabato ni neno
linalotokana na neno la Kiebrania “Shabbat” ambalo lina maana kuacha, au
kupunzika (kustarehe). Kutokana na utaratibu wa Mungu
kulikuwa na Sabato mbili.
Sabato ya
kwanza.
Mungu aliumba vitu
vyote kwa siku sita. Siku ya saba aliacha kufanya kazi akapumzika. Hii ni
sabato kwa ajili Mungu. “Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi
lake lote. Na siku ya saba alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku
ya saba ,akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya
saba, akaitakasa kwa sababu siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi
yake yote aliyoiumba na kuifanya…” Mwanzo 2:1- 4.
Sabato ya pili.
Hii ilikuwa ni
sabato kwa ajili ya wana wa Israeli. Mungu alipowatoa wana wa Israeli utumwani
Misri, kwa kumtumia mtumishi wake Musa, aliwapa amri ya sabato. Sababu ya
kupewa sabato ni ili wamkumbuke Mungu aliwaokoa kutoka utumwani
Misri. “Nawe
utakumbuka ya kuwa wewe ulikuwa utumwani katika nchi ya misri, na yakuwa Bwana,
Mungu wako, alikutoa huko kwa mkono wenye nguvu, na mkono ulionyoshwa; kwa
sababu hiyo Bwana,Mungu wako, alikuamuru uishike sabato.” Kumbukumbu 5:15. Katika sabato hii Mungu alifanya iwe ishara kati
yake na Israeli.
Maana ya neno
ishara.
Neno ishara
linatokana na neno la Kiebrania “ot” ambalo
linamanisha (a) Ishara, alama; (b) Ishara ya ajabu, muujiza. Mungu aliifanya
iwe ni ishara kati yake na wana wa Israeli, kwa sababu baada ya uumbaji
alipumzika kufanya kazi; Imeandikwa: “Ni ishara kati ya mimi na wana Israeli milele; kwani
kwa siku sita Bwana alifanya mbingu na nchi, akastarehe siku ya saba na
kupumzika.” Kutoka 31:17. Mungu aliwaagiza wana wa Israeli
kuitunza sabato.
Maana ya kuitunza sabato.
Siku ya saba wana
Israeli walipaswa kuzingatia kama ifuatavyo: Kuacha kufanya kazi yoyote na
ikiwa mtu aliivunja amri hii aliuawa. Mungu aliwapa agizo kwa kusema, “Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni sabato ya
kustarehe kabisa, takatifu kwa Bwana; kila mtu atakayefanya kazi yoyote katika
siku ya sabato, hakika yake atauawa.” Kutoka 31:15.
Wasiwashe
moto.
Wasingepika
chakula siku ya saba ambayo ni sabato. “Hamtawasha moto katika nyumba zenu kwa siku
ya sabato.” Kutoka 35:3.
Kuhani
kuteketeza sadaka.
Kuhani alikuwa na
ruhusa ya Mungu kufanya kazi ya kuteketeza sadaka. “Tena siku ya sabato watasongezwa
wana-kondoo wawili, waume wa mwaka wa kwanza,wakamilifu pamoja na sehemu
kumi mbili za efa za unga mwembaba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na
mafuta, pamoja na sadaka yake ya kinywaji; hii ndiyo sadaka ya kuteketezwa kila
sabato...” Hesabu
28:9,10.
Sabato wakati wa Agano Jipya.
Agano Jipya ni
kipindi kinachoelezea habari za kuzaliwa, kufa, kufufuka na kupaa kwa
Bwana wetu Yesu Kristo. Katika kipindi hiki hata sasa sheria ya zamani ya
Musa kuhusu sabato ilibatilishwa na kufanywa upya. Ndiyo maana Yesu
alimponya mtu siku ya sabato, akasema “ …Basi ni halali kutenda mema siku ya
sabato” Mathayo 12:12. Alikuwa na mamlaka ya kufanya lilo njema siku ya sabato. Yeye
ndiye aliifanya sabato; kwa kuwa imeandikwa: “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakukufanyika chochote
kilichofanyika.” Yohana 1:3.
Baada ya Yesu
kumpomya mtu siku ya sabato, viongozi wa dini na sheria ya Mungu wakaona
na kufikiri ameivunja sabato. Lakini kwa kutokuyafahamu maandiko hawakumjua
Yesu ni nani. Yesu alikuwa ni Bwana wa sabato na ni kuhani milele, Yesu
akawaambia; “Wala
hamkusoma katika torati, siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato
wasipate hatia? Kwa maana mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato. Kisha
akamwambia yule mtu, nyosha mkono wako; akaunyosha , ukapona, ukawa mzima kama
wa pili.” Mathayo 12:3,8,13.
Je,
wakati wa agano jipya tunatunza sabato?
Katika torati (sheria) iliandikwa mambo mengi ambayo
iliamuru yafuatwe, ambayo yalikuwa ni kivuli cha agano jipya; ndiyo maana
imeandikwa: “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa
sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha
mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.” Wakolosai 2:16,17. Katika haya maandiko, Wakolosai
wanashauriwa ya kwamba mtu asiwahukumu kwa kutokuifuata torati kuhusu vyakula,
vinywaji, sikukuu, mwandamo wa mwezi na sabato.
“Basi, sasa
mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea
mafundisho ya kwanza “torati” yaliyo manyonge, yenye upunguvu, ambayo
mnataka kuyatumikia tena? Mnashika siku, na miezi, na nyakati, na miaka.” Wagalatia 4:9,10. Maandiko
haya yaliwaonya Wagalatia waache mafundisho waliyoyarudia na
kuyatumikia, kwa sababu ni manyonge, yana upunguvu, yasingewakamilisha katika
neno la Mungu. “Maana, kuna kubatiliwa ile amri
iliyotangulia, kwa sababu ya udhaifu wake, na kutokufaa kwake; (kwa maana ile
sheria haikukamilisha neno); …….” Waebrania 7:18,19.
Sabato kukoma.
Yesu aliponya mara
kwa mara siku ya sabato, kwa sababu hiyo isingetunzwa tena. Wakati wa sabato
ulikuwa karibu kwisha kwa sababu amekuja Bwana wa sabato kuikamilisha sheria.
Isingalikuwako tena, ilibatilishwa, ndiyo maana Yesu alifanya kazi siku
ya sabato, akawajibu Wayahudi akasema. “……Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami
ninatenda kazi.” Yohana 5:10,17. Ndiyo maana sasa yatupasa:
Kumwabudu Mungu
katika roho.
“Yesu akamwambia,
Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala
kule Yerusalemu “Hekaluni”. Lakini saa inakuja, na sasa ipo, ambao
waabuduo halisi watamwabudu Baba katika Roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta
watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, na wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu
katika Roho na kweli.” Yohana
Yn 4:21,23-24. Kwa sababu hiyo
tunahesabiwa haki.
Kuhesabiwa haki
kwa imani.
Hivi sasa ni
wakati wa agano jipya, ambalo lilifanyika kwa damu ya Yesu Kristo iliyomwagika
msalabani. Agano hili ni bora kuliko lile la zamani kwa sababu kila amwaminiye
anahesabiwa haki bure. Sii kwa kutenda kwa matendo ya sheria kama kutunza
sabato, kutoa sadaka za dhambi na matendo mengine ambayo sheria iliagiza. “Kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria, ili
kila amwaminiye ahesabiwe haki.” "Lakini sasa haki ya Mungu
imedhihirishwa paspo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya
Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Kristo Yesu kwa wote wamwaminio. Maana
hakuna tofauti;” Warumi 3:21;10:4. Imewekwa wazi ya kwamba haki inapatikana kwa imani
ilishuhudiwa na torati na manabii, huu ni ushahidi wa kutosha. Neno
lolote huthibitika kwa vinywa vya mashahidi zaidi ya mmoja. "... Kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno
lithibitike". Mathayo
18:16.
Umeeleweka saana Mungu akubariki 5
JibuFutaBwana Mungu awabariki kwa mafundisho yenu yenye kutukuza kiroho, AMINA.
JibuFuta