Tutaangalia katika somo hili jinsi Mungu anavyosema na watumishi wake. Kuna njia ambayo Mungu alitumia kusema na wana wa Israel kupitia watumishi wake wakati wa Agano la Kale na Agano Jipya ilikuwa ni kwa njia ya manabii. Mungu alipotaka kusema na wana wa Israel alimtuma nabii na kumwaagiza maneno ambayo atawaambia watu wake. Ndio maana imeandikwa, "Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu". 2 Petro 1:21. Kutokana na andiko hili linaonyesha wazi nabii yampasayo kuzingatia. Jambo la kwanza kwa mkristo au mtumishi aliyeokoka ni lazima atoe unabii kwa mapenzi ya Mungu (yaani kwa matakwa Mungu). Jambo la pili ili mkristo au mtumishi aliyeokoka aweze kutoa unabii ni lazima awe ameongozwa na Roho mtakatifu. Njia hii ni mojawapo tu lakini zipo njia nyingine ambazo Mungu hutumia kusema na watu wake ambazo ni kama ifuatavyo;
1. Kwa njia ya maono na ndoto.
Mtume Paulo alipewa maelekezo na Mungu kupitia maono sehemu ambayo atakwenda kuhubiri. “Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, kumsihi, na kumwambia, vuka, uje Makedonia utusaidie”. Matendo 16:9.
2. Kwa njia ya malaika.
Malaika wa Mungu alimtokea Zakaria ambaye ni Kuhani alipokuwa katika zamu yake ya akivukiza uvumba hekaluni. Mungu alimpa taarifa ya kwamba maombi aliyomwomba Mungu ameyasikia, na kuhusu mtoto atakayezaliwa.
"Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia.
Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana". Luka 1:11-13.
"Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia.
Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana". Luka 1:11-13.
3. Kwa njia ya Yesu Kristo.
“Mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika mwana aliyemwekwa kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.” Waebrania 1:2.
4. Kwa njia ya Roho Mtakatifu.
Mungu alisema na Mitume kupitia Roho Mtakatifu. "Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia.Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa", Matendo 16:6-7. "Na Petro alikuwa akiyafikiri yale maono. Roho akamwambia, Wako watu watatu wanakutafuta. Basi ondoka ushuke ufuatane nao, usione tashwishi, kwa maana ni mimi niliyewatuma". Matendo 10:19,20.
Sababu za kutosikia sauti ya Mungu.
Kuna mambo ambayo ni sababu ya mtu kushindwa kuisikia sauti ya Mungu. Mambo hayo ni haya yafuatayo;
1.Kutozaliwa mara ya pili na kuokoka. Ikiwa mtu hajaokoka hana uhusiano na Mungu. Kwa sababu hiyo hawezi kuisikia sauti ya Mungu.
2. Kutosamehe waliokukosea na kuweka kinyongo, chuki na uadui.
3. Kuisha katika dhambi.
Maisha ya dhambi ni pale mtu anaposema uongo, usengenyaji, wivu, chuki, kinyongo, uadui, mawazo mabaya, dharau, kujivuna, kujisifu, kujiona bora kuliko wengine, ubaguzi, kutamani mke au mume wa mtu mwingine, na mambo mengine yote yasiyompendeza Mungu.
Mungu huongea kwa kusudi maalumu.
Siyo kila wakati Mungu anasema na watu wake, bali hufanya hivyo kwa kusudi lake na kwa uhitaji wa mtu kwa yale ambayo anamwomba au kumwuliza Mungu jambo fulani ambalo anahitaji jibu kutoka kwake.
Sababu ya pili. Mungu husema kwa ajili ya kuwaonya watu wake ikiwa wameishi maisha ya dhambi ili waweze kumgeukia yeye kwa njia ya kutubu na kuziacha dhambi zao na kuwapa maelekezo namna ya kuishi sawasawa na neno lake asije akawahukumu.
Sababu ya tatu. Mungu husema na watu wake kwa ajili ya kufariji na kutia moyo kutokana na dhiki na shida wanazopitia katika maisha yao.
Sababu ya nne. Mungu anaweza kusema kwa ajili ya kusudi lake maalumu. Kusudi hilo linaweza kuwa kwa ajili ya mtu binafsi, Kanisa, Taifa au ulimwengu.
Tahadhari kuhusu kusikia sauti, kuota ndoto, kuona maono na unabii.
Jambo muhimu kwa kanisa na watumishi wa Mungu ni kuwa makini wasiamini kila sauti watakayoisikia kwa sababu si kila sauti inatokana na Mungu. Wakati mwingine huwa ni sauti ya shetani na malaika zake ambao waliomwasi Mungu na kupoteza nafasi zao Mbinguni. Ndio maana tukisoma maandiko tunaweza kuona shetani alivyosema na Hawa na kumdanganya ale matunda aliyokatazwa na Mungu asile. ”Nyoka akamwambia mwanamke. Hakika, hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya... Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula...Alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.“ Mwanzo 3:4-6.
Kuhusu ndoto ni muhimu kuwa makini kwa sababu kuna ndoto zinazotokana na fikra au mawazo ambayo yanatokana na mambo uliyoyaona, kuyasikia au kuyahisi. “Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi; na sauti ya mpumbavu kwa njia ya wingi wa maneno” Mhubiri 5:3. Vilevile mtu anaweza kuota ndoto ambazo hutokana na Shetani kwa sababu anaisha maisha ya dhambi. Huweza kuota ndoto ambazo ni mbaya, za kutisha na mateso.
Pia kuhusu maono. Sii maono yote yanatokana na Mungu, bali mengine yaweza kutoka kwa shetani. Tukisoma katika biblia kuna andiko linalohusu mwanamke mchawi aliyemwona nabii Samweli ambaye alikuwa amekufa siku nyingi zilizopita kwa njia ya shetani. Ilikuwa ni baada ya Sauli kumwendea ili ambashirie “Yule mwanamke akamwambia Sauli, Ninaona mungu anatoka katika nchi naye akamuuliza ni mfano wa nini? Akamjibu, Ni mzee anazuka; naye amefunikwa vazi. Basi Sauli akatambua ya kwamba ndiye Samweli mwenyewe…” 1Samweli 28:13.
Sehemu nyingine tunaweza kuona shetani alipomjia Yesu ili kumjaribu na kwa muda mfupi alimwonyesha utajiri wote wa dunia hii. “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia. Ndipo Yesu akamwambia, Nenda zako, Shetani, kwa maana imeandikwa, msujudie Bwana Mungu wako umwabudu yeye peke yake. Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia." (Mathayo 4:8-11).
Kuhusu unabii. Unabii wowote unaotolewa unapaswa kupimwa ndipo kuuthibitisha kama umetokana na Mungu. Kuhusu sehemu hii nitaelezea unabii uliotolewa na manabii ambao waliingiwa na pepo wabaya kwa ajili ya kutabiri uongo na hatimaye Ahabu alidangaywa ili auwawe vitani. Wale pepo walimwambia Mungu, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo vinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka, ukafanye hivyo. 2Nyakati 18:22.
Kupima unabii, ndoto na maono kwa usahihi ni kwa njia zifuatazo;
- Neno la Mungu.
- Roho Mtakatifu.
1. Awe anayafahamu maneno ya Mungu kwa ukamilifu
2. Awe anadumu katika utakatifu kwa kuishi sawasawa na maneno ya Mungu yanayosema.
3. Awe amejazwa Roho mtakatifu
Mambo hayo matatu ni muhimu sana kwa kanisa. Ikiwa mtu amekamilika katika mambo hayo anaweza kupambanua na kuthibitisha ya kuwa unabii, ndoto na maono yametokana na Mungu au shetani.
Ili kufahamu zaidi bofya hapa: Jinsi ya kuwatambua manabii wa kweli.
Mungu akubariki sana
JibuFutaNimebarikiwa sana
Mfano mzuri ambao Yesu mwenyewe alishuka akiongea na mtu ni pale alipo mkemea sauli ambaye ni paulo
JibuFutaBarikiwa
JibuFutaUBARIKIWE MNOO
JibuFuta