Ruka hadi kwenye maudhui makuu

MATUMIZI SAHIHI YA DAMU YA YESU.

Ili mtu ajue matumizi sahihi ya damu ya Yesu ni muhimu aangalie  neno la Mungu linavyosema. pia kwa kila jambo ambalo mtu analitenda ni muhimu kwanza kulithibitisha kwa kutumia neno la Mungu na kuona kama linaendana sawasawa na maandiko. Kwa hiyo jambo lolote linalopingana na neno la Mungu sii halali kulifanya. Ikiwa mtu atatenda jambo lolote lililo kinyume na neno la Mungu atakuwa amefanya dhambi.  Kwa sababu hiyo yampasa kila mmoja aliyeokoka kujua matumizi sahihi ya damu ya Yesu sawasawa na neno la Mungu.

Matumizi ya damu Yesu ni haya yafuatayo:
1. Kuosha dhambi za ulimwengu. Ndio maana andiko linasema,"Bali tukieneda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake yatusafisha dhambi zetu. 1Yohana 1:7." "Hao ndio watokao katika dhiki iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo (Yesu) . Ufunuo 7:14."

2. Kanisa limenunuliwa kwa damu ya Yesu.Ndio maana imeandikwa, " Nanyi mfahamu ya kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au kwa dhahabu...bali kwa damu ya thamani, kama ya Mwana-Kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo. 1Petro 1:18-19." "...Kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa. Ufunuo wa Yohana 5:9."

3. Kuondoa dhambi ya ulimwengu.
Ndio maana Yesu alikuja kama Mwana-Kondoo kwa ajili ya dhambi za ulimwengu na damu yake ilimwagika pale msalabani. Kwa sababu hiyo Yesu akasema, "Kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. Mathayo 26:28." Andiko linginge linaonyesha wakati Yohana mbatizaji alipomwona Yesu alimthibitisha akasema, "...Tazama, Mwana-kondoo wa  Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu". Yohana 1:29."
"Naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote" 1Yohana 2:2." "Na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote kwa nafsi yake, akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni. Wakolosai 1:20." 
Katika  maandiko hayo yanaonyesha Yesu ndiye anayempatanisha mtu mwenye dhambi na Mungu. Ni pale mtu anapomgeukia Mungu kwa kuweka nia moyoni mwake kuachana na dhambi, kumwamini Yesu na kutubu. 

Yesu alikufa mara moja.
Imeandikwa, "Maana kwa kule kufa kwake, aliifia dhambi mara moja tu; ...Warumi 6:10." Kwa sababu Yesu alikufa mara moja, pia damu yake ilimwagika mata moja, wala haikumwagika kila siku. Bali kwa damu ya Yesu watu wanapata ondoleo la dhambi zao. Kwa sababu hiyo kuitumia damu ya Yesu kwa namna nyingine sii sahihi. Katika neno la Mungu hakuna mahali  popote ambapo Mungu anatoa ruhusa kuitumia kwa namna nyingine. Kwa sababu hiyo kuitumia katika kuombea mtu kwa kusema damu ya Yesu imfunike na kumlinda. Ifunike biashara yake, ifunike watoto wake. Kuomba au  kusema ninanyunyiza damu ya Yesu katika nyumba hii, ninanyunyiza damu ya Yesu katika biashara hii. Kuomba kwa namna hiyo ni  kinyume na neno la Mungu. Na si hivyo tu, ikiwa mtu anaitumia damu ya Yesu kama ulinzi kwa kusema kwa damu ya Yesu najifunika, au damu ya Yesu ilinde  nyumba hii au gari hili, haya sii matumizi ya damu ya Yesu.

Damu ya Yesu ni kwa ajili ya kumtakasa mtu na kumweka wakfu kwa Mungu. Kulingana na neno la Mungu wakati wa agano la kale imeandikwa karibu vitu vyote vilitakaswa kwa damu sawa sawa na sheria ya Mungu. "Maana kila amri lipokwisha kunenwa na Musa kwa hao watu wote, kama ilivyomuru sheria, aliitwaa damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji na sufu nyekundu na hisopo, akakinyunyizia kitabu chenyewe, na watu wote, akisema, Hii ni damu ya agano mliloamriwa na Mungu. Na ile hema nayo na vyombo vyote vya ibada alivinyunyizia damu vivyo hivyo. Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo, Waebrania 9:19-22." Kwa sababu hiyo   tunasafishwa na kuondolewa  dhambi. 

Baada ya kuelezea kazi au matumizi ya damu ya Yesu. 
Kuhusu ulinzi wetu neno la Mungu linasema "Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani...1Petro 2:5." 
Pia imeandikwa,"Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa. Zaburi 34:7."
Kwa hiyo kutokana na maandiko haya yanaonyesha wazi tunalindwa na NGUVU ZA MUNGU na MALAIKA.

Ndugu zangu katika Bwana ninawasihi kwa jina la Yesu Kristo yatupasa kufahamu kuomba sawasawa na neno la Mungu. Na kufamya yote sawasawa na neno lake. 

Mungu Baba yetu katika Jina la Yesu atujalie nuru ya ufahamu katika mioyo yetu ili tufahamu jinsi itupasavyo kuomba na kufanya yote katika mapenzi yake. Amen.

Maoni

  1. Amina mtumishi wa mungu.Endelea kujifunza zaidi kuhusu damu ya Yesu kimatumizi.

    JibuFuta
  2. Bila jina10:47

    Barikiwa Sana

    JibuFuta
  3. Bila jina22:22

    Amina sana mtumishi hapa nmezidi kuongeza maarifa zaidi

    JibuFuta
  4. Bila jina08:45

    Nimejifunza na kuelewa umuhimu wa Damu ya Yesu

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

KUMTUMIKIA MUNGU KWA BIDII.

Kutokana na kichwa cha somo hapa juu katika matukio wazi ili mtu amtumikie Mungu ni lazima awe na bidii. Kwa sababu hiyo kwa mtu yule ambaye ameweka nia moyoni mwake ya kwamba atatumikia Mungu kwa bidii. Tukiangalia kuhusu mwanadamu kuna mambo mengi katika maisha yake ameyafanya kutokana na bidii aliyo nayo. Lakini ikiwa mtu hana bidii kwa ajili ya mambo ya Mungu kamwe hawezi kuingia ufalme wa Mungu. Ndio maana imeandikwa;  "Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatimkana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka,   Mathayo 11:12 ."    " Torati na manabii vilikuwapo mpaka Yohana; tangu wakati huo habari njema ya ufalme wa Mungu hutangazwa, na kila mtu hujiingiza kwa nguvu."   Luka 16:16. Hapa ninatoa ushuhuda wangu binafsi, kuhusu kumtumikia Mungu kwa bidii. Wakati nilipookoka nilikuwa na kiu au shauku kwa ajili ya kutaka kujazwa Roho Mtakatifu. Kwa sababu nilikuwa ninamhitaji sana nilimwomba mtumishi mmoja wa Mungu aniombee ili niweze kujazwa...

KUISHI MAISHA YA UTAKATIFU.

Utakatifu  - Ni maisha ya Mkristo anayoyaishi kwa kuzingatia kanuni ya neno la Mungu baada ya kumkiri na kumpokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake. Kuishi maisha ya utakatifu ni jambo linalowezekana, kwa sababu Mungu alipomuumba mwanadamu alimwekea hiari ndani yake kwa kutokea kwa tukio. Ndio maana Yesu alipokuwa akifundisha alitumia mfano wa mti kuonyesha mtu anavyoweza kuishi maisha haya ya kumpendeza Mungu au ya maisha ya dhambi. "   "Ufanye mti kuwa mzuri na matunda yake kuwa mazuri, au ufanye mti kuwa mbaya na matunda yake mabaya, kwa maana kwa matunda yake mti hutambulikana" Mathayo 12:33. Kuishi maisha ya utakatifu ni agizo la Mungu kwa wale wote aliowachagua. Ndio maana Mungu alimwambia Musa,   "Nena na makutano wote na wana wa Israel, uwaambie, mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana Mungu wenu ni mtakatifu"  Walawi    19:2. Kuwa mtakatifu ni kumpendeza Mungu, kwa sababu amesema;  “Watakatifu waliopo duniani ndio walio bora...

TUNDA LA UAMINIFU.

Uaminifu ni mojawapo ya tunda la Roho katika maandiko matakatifu. Tutajifunza uaminifu wa Mungu unaopatikana katika neno lake. Yeye amesema atatimiza yale aliyoahidi katika neno lake, si tu kwa wana wa Israel bali kwa watu    wote wanaoishi sawasawa na neno lake. Kwa hiyo, kwa upande wetu inatupasa sisi nasi kuwa waaminifu kwa kuliishi na kulitenda neno la Mungu.   “Basi jueni ya kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye Mungu; Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake, hata vizazi elfu.   Na itakuwa, kwa sababu mwazisikiza hukumu hizi, na kuzishika na kuzitenda, basi Bwana, Mungu wako, atakutimizia agano na rehema aliyowaapia baba zako.”   Kum 7:9, 12.   “Ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu    halitanirudia bure bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.   Isa 55:11" Tabia ya mtu mwaminifu. 1. Mtu aliye mwaminifu ni yule ambaye anatenda sawa...