Tunaweza kuona ya kwamba vitu vyote ambavyo Mungu ameviumba ni muujiza kwetu. Pia aliumba kwa namna ya pekee jua, mwezi, nyota na sayari nyingine mbalimbali ambazo aliziweka juu ya anga, huku zikiwa zinaning’inia bila kushikiliwa na kitu chochote, wala hazidondoki. Pia bahari nayo imekaa mahali ilipoamriwa bila kuvuka mpaka alioiwekea Bwana. Kwa hiyo tunapoona uumbaji wa vitu vyote ambavyo Mungu aliviumba vinashangaza, navyo ni ishara kwetu ya kutosha na kutambua ya kwamba Mungu yupo. Kwa sababu hiyo yatupasa kufahamu ya kwamba yeye ndiye mwenye uwezo wote, yeye hutenda mambo yote sawasawa na mapenzi yake. Kwa hiyo tunaweza kuona Sababu ya Mungu kufanya muujiza kwa mkono wa Musa mbele ya Farao na Wamisri. Mungu akamwambia Farao; “lakini, nilikusimamisha wewe kwa sababu hii hii, ili nikuonyeshe uweza wangu, tena kwamba jina langu litangazwe katika dunia yote.” Kutoka 9:16. Kutokana na andiko hili hapa juu linazungumzia Mungu alifanya miujiza ili kumwonyesha Farao uweza wake. Na Kusudi lingine ni ili jina la Mungu litangazwe duniani kote. Ndio maana hata sasa Jina la Mungu linatangazwa ulimwengu kutokana na matendo makuu aliyoyatenda kwa nyakati tofauti.
Pia yatupasa kutambua ya kwamba Mungu ndiye atendaye miujiza yote. Kwa sababu hiyo hakuna mtu mwenye uwezo wa kufanya muujiza. Ndio maana mtume petro aliwahutubia Waisraeli akawaambia; “Enyi waume wa Israeli, sikilizeni maneno haya: Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua;” Matendo ya Mitume 2:22. Hili andiko hapa juu linamaanisha ya kwamba Mungu alifanya miujiza, ajabu na ishara kwa mkono wa Yesu Kristo. Kwa hiyo Mungu alimtumia kufanya matendo ya miujiza.
Kwa sababu hiyo yawapasa waliookoka kuwa makini na kufahamu kuna kanuni na mwongozo wa neno la Mungu kuhusu kufanya muujiza. Katika kanisa kuna baadhi ya wakristo ambao wamejaliwa kuwa na karama ya muujiza. Wanaweza kutumiwa na Mungu ikiwa watafuata kanuni na mwongozo wa neno la Mungu linavyosema. Kwa hiyo mtu anaweza kufanya muujiza kwa mapenzi ya Mungu na kuongozwa na Roho wa Mungu. Kwa sababu hiyo mtu hawezi kufanya muujiza kwa matakwa yake au kama yeye apendavyo. Lakini kama mtu atataka kufanya muujiza kwa matakwa yake haiwezi kutokea. Ila kwa mtu aliye mnyenyekevu na kutaka mapenzi ya Mungu yatimizwe, huyo ndiye hutenda miujiza kwa imani na kuongozwa na Roho Mtakatifu.
Mambo yakuzingatia ili mtu aweze kutumiwa na Mungu katika maisha yake ni haya yafuatayo;
1.Kudumu katika utakatifu. Hii ndiyo njia ambayo inampendekeza Mungu. Ndio maana Mungu amesema, “Watakatifu waliopo duniani ndio Walio bora, Hao ndio niliopendezwa nao.” Zaburi 16:3.
2. Kumwomba Mungu siku zote.
3. Kumsifu na kumwabudu Mungu.
4. Kufunga mara kwa mara.
5. Kuyatoa maisha yako kwa ajili ya Mungu na kumhofu yeye. Kufanya hivyo ni Jambo la msingi katika kumtumikia Mungu. Ndivyo Bwana wetu Yesu kristo alifanya, yeye ni kielelezo katika maisha yetu. Imeandikwa “Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu;” Waebrania 5:7. Andiko hili limeonyesha wazi ya kuwa Yesu alimtolea Mungu mwili wake na kumhofu.
6. Kunyenyekea.
Kutokana na fundisho hili ninashauri ya kwamba mtu ambaye anatumiwa na Mungu kwa karama ya miujiza awe makini asije akampa mtu tumaini ya kwamba Mungu atafanyia muujiza fulani, wakati Mungu hajamthibitishia hivyo. Kuna mtumishi mmoja alikuwa anahubiri katika kanisa fulani. Katika kanisa hilo kulikuwa na mama mmoja ambaye hajafanikiwa kuwa na mtoto. Yule mtumishi akamwambia yule mama majira kama haya mwaka ujao utakuwa na mtoto, lakini haikuwa kama alivyomwahidi. Kwa sababu hiyo yule mama alipewa tumaini ambalo si kweli.
Kwa hiyo si sahihi kuwatangazia watu wenye shida mbalimbali waje kanisani au kwenye mkutano wa injili na Bwana atawaponya na kuwaweka huru. Ni muhimu kutambua ya kwamba kuna kusudi kuu la Mungu ambalo ni kuhubiri habari njema (injili). Kwa hiyo hilo ndilo kusudi kuu la Mungu kwa watu wake. Kwa sababu hiyo mtumishi wa Mungu akiwa anahubiri habari njema ya ufalme wa Mungu kwa usahihi na huku akiwa amedumu katika neno la Mungu. Mtu wa namna hiyo neema ya Mungu inakuwa juu yake kwa ajili ya kulithibitisha neno la Mungu kwa ishara na maajabu. Tunaweza kuona kupitia wale mitume, imeandikwa;
“Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.]” Marko 16:20.
“Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.]” Marko 16:20.
Kuepuka mazoea.
Kwa mtu aliye na karama ya miujiza. Ni muhimu kufahamu ya kwamba si kila mara Mungu atamtumia kutenda miujiza. Yeye Mungu hutenda kwa wakati na kwa kusudi maalum. Kwa mfano kama miujiza imetendeka katika mji fulani, lakini si lazima itendeke mji mwingine kwa sababu inategemea mapenzi ya Mungu.
Pia inategemea imani na utii kwa wale wanaohubiriwa habari njema. Hapa ngoja nikupe mfano ili uweze kuelewa. Kulikuwa na watu kumi ambao waliokuwa na ukoma walimwendea Yesu huku wakiamini angeweza kuwaponya. Lakini aliwapa agizo wakajionyeshe kwa Kuhani. Walipokuwa njiani wanaelekea kwa Kuhani walipona. Waweze kuona kwa sababu ya imani yao na kutii agizo walilopewa ndio maana walipona. “Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu! Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika.”
Luka 17:12-14. Vilevile kulikuwa na mtu aliyepooza naye akapewa agizo. “Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako uende nyumbani kwako. Mara akaondoka, akajitwika godoro lake, akatoka mbele yao wote; hata wakastaajabu wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Namna hii hatujapata kuiona kamwe.” Marko 2:11-12. Kwa hiyo pasipo imani na utii hakuna muujiza kutoka kwa Mungu.
Maoni
Chapisha Maoni