Ruka hadi kwenye maudhui makuu

USHUHUDA WA MAONO YA MBINNGUNI NA JEHANUM. NA NYISAKI CHAULA.

Huu ni ushuhuda wa maono juu ya mbinguni na Jehanamu uliotolewa na mwanamke Nyisaki Chaula.  Nyisaki Chaula ni mtumishi wa Mungu, mkazi wa mkoa wa Mbeya nchni Tanzania Yesu Kristo aliye hai alimchukua na kumwonyesha maono hayo, na ilikuwa mwezi desemba mwaka 1991. Yesu Kristo alimpa maono hayo, akamwagiza aandike na kushuhudia maono hayo kwa kanisa lake na watu wote, ili kila mwanadamu apate kufahamu uhalisi wa mbinguni na Jehanamu, makao yanayowasubiri wanadamu wote baada ya maisha ya hapa duniani.
Hii si habari ya kutungwa, ni jambo la kweli ambalo lilitokea. Usome ujumbe huu kwa moyo uliofunguka, huku ukimwomba Mungu akuwezeshe kuuelewa na pia kuwaeleza wengine.
Ujumbe huu umenukuliwa kama ulivyoandikwa na mwanamke Nyisaki Chaula mwenyewe, ambaye alionyeshwa maono haya!
USHUHUDA WA MAONO YA JEHANAMU.
NA NYISAKI CHAULA.
UYOLE – MBEYA, TANZANIA
.


UTANGULIZI
Nduguyangu kuna shuhuda nyingi sana zinazoletwa duniani, kuhusu mbinguni na jehanamu, lakini ni watu wachache wanaozingatia na kuziamini; kwa vile watoaji washuhuda hizo si wa dini zao au si wa madhehebu yao na hawajulikani makanisani. Sasa ninakuomba wewe msomaji, tafuta mahali penye utulivu, mwombe Mungu na unapousoma ushuhuda huu ili upokee kile ambacho Bwana amekuletea siku ya leo.
Msichana Nyisaki Chaula alionyeshwa na Bwana ushuhuda huu akiwa na umri wa miaka 16 mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi. Ushuhuda huu alionyeshwa akiwa amempokea Yesu Kristo (kuokoka).  Si kwamba alikufa bali alionyeshwa maono na Bwana. Maono haya alionyeshwa kati ya tarehe 30 na 31/12/1991; yaani kwa siku mbili tofauti.
Msichana huyu hivi sasa ameolewa na Mwinjilistii Lemsy Mheni pale Uyole, mkoa wa Mbeya, nchini Tanzania,  kwa lengo la kukuza huduma yao. Kabila lake ni Mkinga wa Makete, msichana huyu anapatikana Uyole njia panda ya Malawi – Zambia na Dar es Salaam pembeni mwa kituo cha mafuta ya magari pale Uyole. Mungu akutangulie unapousoma ujumbe huu, upate kuuelewa na kuupokea kwa Jina la Yesu Kristo. Amen.                                                  
SURA YA 1
KUITWA NA BWANA YESU KRISTO
Ilikuwa ni mwezi wa 12 mwaka 1991, tulipochaguliwa vijana 10 kuombea Mkutano wa Kiroho ambao ulikuwa ukifanyika pale Uyole – Mbeya. Siku moja baada ya maombi ya usiku, nililala pamoja na dada zangu. Siku hiyo nililala usingizi mzito ambao sijapata kuuona. Usiku nilishangaa kukuta usingizi umetoweka kabisa, hivyo nikabaki nikiwa macho, ndipo nikasikia sauti ikiita Nyisaki, nikasikia lakini sikuitika, ikaita mara ya pili pia sikuitika. Hata mara ya tatu ndipo nikaitika kisha nikasikia ile sauti ikisema, “Nimekuchagua kuwa mtumishi wangu, ndipo nikatambua kuwa ni sauti ya Bwana.  Nikasema Ee Bwana mimi ni mtoto mdogo tena hata chuo chochote sijaenda nitawezaje kuifanya kazi hiyo!  Bwana akaniambia mkumbuke Yeremia mtumishi wangu nilimchagua angali bado mdogo (Yeremia 1:5) basi nikaendelea kubishana na ile sauti hadi dada yangu mmoja aliamka na kusema Mshukuru Mungu kwa sababu amekuchagua wewe.
Ndugu msomaji kumbuka kuwa sauti hiyo nilisikia nikiwa macho kabisa na wala haikuwa ndoto na baada ya kusikia sauti hiyo mara ya kwanza na ya pili niliamka na kuthibitisha kabisa kuwa wote niliokuwa nimelala nao bado wamelala. Na hata huyo dada yangu aliyesema Mshukuru Mungu kwa sababu amekuchagua wewe nilitambua kuwa ni Mungu ndiye aliyemuelimisha na kumfunulia jambo hili.B Baadaya hayo yote tukamshukuru Mungu na kulala. Kesho yake tarehe 30/12/1991 ndipo nilipoonyeshwa mambo makuu ya ajabu (Yeremia 33:3)
SURA YA 2
JEHANAMU– SEHEMU YA KWANZA NA MANGOJEO YA WAFUI
Ilikuwani tarehe 30/12/1191, nasi tuliamka, tukaenda kwenye semina na baada ya ile semina tuliamua kwenda kumuona rafiki yetu aliyempokea Yesu (kuokoka) ambaye kwa muda ule alikuwa hajiwezi yaani alikuwa anaumwa. Tulipofika pale nyumbani tukafungua ibada kwa maombi kisha tukaanza kujifunza jinsi Biblia inavyosema kwa njia ya maswali. Hata baada ya hapo tukaamua kufunga ibada yetu kwa maombi kama tulivyofungua.
Tufunge kwa maombi na kumkabidhi ndugu yetu mikononi mwa Bwana, maana tulianza ibada yetu kwa kumshukuru Mungu kwa kuwa ndugu yetu alikuwa anaendelea vizuri.  Ninachokumbuka ni kwamba tuliimba wimbo mmoja wa kuabudu, lakini sikumbuki kama tuliingia kwenye maombi au la tulipokuwa tunaimba ule wimbo wa kuabudu, nikashangaa kuona kuwa mimi nimechukuliwa, na niko sehemu tofauti kabisa na mazingira ya pale nyumbani.
Ukiniuliza kuwa nilichukuliwa vipi hata mimi mwenyewe sielewi, lakini nilishangaa kuona kwamba niko kwenye bonde moja kubwa sana, na lile bonde lilikuwa halina miti wala majani wala ndege na vitu vilivyopo duniani, sehemu yenyewe ilikuwa haivutii hata kidogo, ni sehemu moja iliyokuwa na ukimya wa aina yake. Sasa nikashangaa kwa kuwa nilikuwa na rafiki zangu na sasa siwaoni, nikaendelea kujiuliza ni nani aliyenileta huku, na hapa ni wapi?
Basi niliamua moyoni mwangu kuwa jambo lolote likalotokea na litokee, kwa sababu hata sijui aliyenileta mahali hapa. Nilikuwa nimekata tamaa, nikajiandaa kutaka kukaa, ndipo nikasikia sauti nyumba yangu ikisema Nyisaki nifuate. Nilipoinuka nilishangaa sana kumuona Mtu mmoja mfano wa mwanadamu; nilipomtazama yule Mtu, umbo lake hakuwa mrefu sana wala hakuwa mnene sana, alikuwa ni mtu ambaye sijawahi kumwona popote duniani. Nywele zake zilikuwa ndefu na alikuwa amezibana nyuma kwa banio jekundu, alikuwa amevaa vazi refu mpaka miguuni na jeupe sana ambalo hata weupe wake sijawahi kuuona hapa duniani.
Alikuwa ni mweupe sana, siyo weupe wa hapa duniani, macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, huyo Mtu alikuwa hakanyagi chini bali alikuwa akitembea hewani na vazi lile lilikuwa liking’aa sana, hata haliwezi kabisa kutazamika kwa macho ya binadamu. Ninasema mambo ambayo niliagizwa niyaseme, huyu Mtu alikuwa amejifunga mkanda mmoja mwekundu kiunoni. Basi nikaamka nikaanza kumfuata (baada ya kusema nifuate). Baada ya hatua chache nikaanza kusikia ngurumo Fulani ambazo zilinitisha kwa kiasi fulani lakini sikuuliza. Kadiri tulivyozidi kutembea mbele ndivyo ngurumo zilivyozidi kuongezeka na kutisha zaidi, mara nikasikia sauti ndani yangu ikiniambia, “inua macho na tazama mbele”, ndipo nikashituka sana nilipoona moshi mkubwa mnene na mweusi umefunika bonde lile na kusababisha giza nene katika bonde lile.
Nikamuuliza yule Mtu huko mbele kuna nini. Yule mtu akasema, hiyo ni Sehemu ya Jehanamu watakakokwenda watenda dhambi baada ya maisha ya duniani. Baada ya kusikia hayo yote ndipo nguvu zikaniishia mwilini mwangu, nikaanza kulia na kumwomba sana Mungu anisamehe maana kwa mawazo yangu nilifikiri kuwa nimekufa na sasa ninapelekwa Jehanamu; nikaendelea kulia sana hadi yule Mtu aliponieleza usilie maana ukilia utashindwa kuwafikishia watu wangu habari hizi. Hofu ilijaa, nilitishika mno, lakini mpango/kusudi la Mungu kunionyesha mambo haya ni ili kuwaambia watu walioko duniani.
Ndugu msomaji, kweli Jehanamu inapoelezwa kuwa ni ziwa la moto, elewa hivyo kuwa ni kweli. Nilipotazama sikuona mwisho wake, Bali niliona milipuko mikubwa sana na ya kutisha na milipuko hiyo haikufanana na milipuko yoyote hapo duniani labda kwa sehemu inaweza kulinganishwa na milipuko ya visima vya mafuta.
Milipuko hiyo ni mikubwa na inatisha mno na ilisababisha moshi mkubwa sana ulioambatana na moto kupaa juu. Moto ule ulijichanganya changanya kama vile bahari iliyochafuka. Kulikuwa na mawimbi makubwa na ya kutisha, yakichanganyika na kutoa ngurumo kubwa ambazo humfanya mwanadamu ashindwe kusikia hata mateso ya mwenzake. Mimi nilipokuwa nasikia na kuhubiriwa habari ya Jehanamu nilifikiri labda ni moto mdogo au makaa ya moto. Lakini siku hiyo nilipoona mwenyewe, niliogopa sana, kiasi kwamba nilibaki kulia na kuomboleza kwa uchungu mkubwa mno. Mtu yule alifanya kazi ya kunionya nisillie, pia alinitia nguvu na ndipo nilipoweza kuendelea, ndugu yangu ukisikia Jehanamu iogope maana inatisha sana.
Nilipoangalia ndani ya ule moto niliona vitu vyenye uhai virefu, vyeupe nikauliza hivyo ni vitu gani? Yule Mtu akasema hao ni funza wa Jehanamu, nikauliza,  hizo rangi kwenye pingili zake ni za nini? Akasema hizo siyo rangi, kama unavyowaona hao funza wana meno hayo manne yenye uwezo hata wa kutoboa fuvu la kichwa cha mtu, na huyo funza akishaingia ndani huacha sumu kali (ndiyo hiyo unayoiona kama rangi, sumu hiyo humtesa mwanadamu milele na milele.)
Hao funza walikuwa ni wengi sana lakini pia hawafi ndani ya ule moto mkali,soma  (Marko 9:45-46). Walikuwa wembamba, warefu yapata mita moja hivi, na walikuwa na pingili pingili ambazo zilionekana kuwa na rangi, walikuwa na meno mawili mbele na pia  kichwani kulikuwa na meno mawili, jumla ya meno yote ni manne, yaani mkiani na kichwani kulikuwa na midomo.
Bwana akasema hawafi wala hawangui kwa sababu wamehifadhiwa kwa ajili ya mateso ya watendao maovu.
Ndugu msomaji, nisingeweza kupoteza muda wangu kukuletea jambo hili, kama sikuliona na kulishuhudia mwenyewe. Ninayasema maneno haya ili ukiwa na sikio, uyasikie maneno haya, ukikataa ni juu yako mwenyewe. Maana sikuagizwa kwamba nimlazimishe mtu ampokee Yesu na kutubu (kuokoka), bali niliambiwa nikamwambie kila mtu, labda atakuwepo mmoja atakayegeuka na kuponywa. Sasa nikauliza mbona watu wanasema Jehanamu kuna watu wanaoungua lakini iweje Jehanamu hii haina watu!  Akasema wanasema kweli lakini watu watakuja kutupwa kwa wakati wake. Lakini muda huu wamehifadhiwa wakimsubiri baba yao aliyewadanganya (yaani shetani).
Akasema twende nikakuonyeshe, nami nikaanza kumfuata. Kweli ndugu zangu Jehanamu uisikie kama ilivyo. Nilipofikiri habari za wale funza wa ajabu kwa kweli nililia kwa uchungu mkubwa mno nilitetemeka na kuishiwa nguvu nikaanza kuwaza moyoni mwangu mtu anayejua dhambi ni mbaya, na anajua neema ya Mungu na kuipuuzia,  kweli uje kuteswa katika ziwa hili la kutisha lenye moto usiozimika na funza ambao hawafi,ni hatari mno,  kwa kweli nililia sana. Lakini yule Mtu akaniambia nyamaza, maana ukilia utashindwa kuyafikisha yote ninayotaka kukuonyesha. Kwa kweli nashindwa hata nieleze vipi. Jehanamu ni kweli ipo na inatisha sana; ninakushauri uyakatae mafundisho ya mashetani yanayosema hakuna Mungu naa kuwa hakuna Jehanamu, ukiendelea kuyafuata hayo mafundisho utaangamia na kujuta milele. Ninaeleza haya ndugu yangu, Mungu hapendi upotee ndiyo maana amekupa nafasi ya kusoma ujumbe huu. Na inawezekana ni nafasi ya mwisho kwako, sasa usipokubali kutubu na kumfuata Yesu Kristo, yawezekana ukajiletea maangamizi wewe mwenyewe.
JEHANAMU IMEANDALIWA KWA AJILI YA SHETANI NA MALAIKA ZAKE
Tuliondokasehemu hii ya Jehanamu na kuelekea sehemu ya mangojeo nikiwa nalia kwa uchungu mkubwa mno. Na haya ninayokuambia sikutishi bali nakuambia kweli na kama unafikiri nakutisha basi utakwenda kuona mwenyewe (usipomfuata Yesu Kristo).
Nikaendelea kumfuata yule Mtu, tulipofika mahali fulani na kutazama bondeni niliona bonde kubwa lililokuwa limefunikwa na giza la kutisha mno. Kabla ya kulikaribia lile bonde, nilisikia sauti za watu zikilia kwa uchungu mkubwa mno. Ndugu yangu kweli Jehanamu kuna vilio vya aina yake, vilio ambavyo huwezi kulia kama walivyokuwa wakilia wale watu, wanalia bila kupumzika. Lile giza nene mno linawafanya wale watu wasiweze hata kutazamana, kila mmoja na kilio chake na kila mtu na mateso yake. Hakuna mtu anayekwenda kumfariji rafiki yake, Kwa sababu kila mmoja aliomboleza kwa ajili ya mateso yake.  kadiri tulivyozidi kuteremka katika lile bonde ndivyo lile giza lilivyozidi kutoweka.
Ndipo tulipofika kule bondeni, nami niliona watu wengi mno wasio na idadi, ni wengi sana na wote walikuwa weusi sana; hakuna mzungu wala mwafrika, wote ni weusi kupita kawaida. Na weusi ulisababishwa na baridi kali sana inayopatikana sehemu ile. Na ndimi zao zilikuwa zimevutwa hadi kufikia kila mtu kifuani pake, awe mrefu au mfupi. Nikauliza mbona ndimi za watu hawa zinafika kifuani? Yule Mtu akasema kama unavyoona sehemu hii haina maji wala haina furaha yoyote, sasa hizo ndimi wanazitumia kwa kulamba machozi, machozi haya hupatikana kwa kilio cha miezi mingi sana kupita na ndipo linatokea chozi moja ambalo hulitumia kama maji. Ndipo nikashikwa na uchungu wa ajabu nikakumbuka hawa ni watu walioishi chini ya Neema ya Mungu walipokuwa duniani, lakini baada ya kufa kwao wako sehemu ya Jehanamu wakimsubiri baba yao aliyewadanganya (shetani). Kulikuwa na wanawake na wanaume wengi sana.
Watu wale walikuwa wakilia kwa uchungu mkubwa mno. Nikamwomba yule Mtu, nikisema Bwana naomba wachukue watu 100 kutoka kila nchi ili waone hii Jehanamu wawaambie wanadamu nao watageuka. Akasema wanadamu ni wenye mioyo migumu hata angerudi Yesu Kristo mwenyewe wasingemwamini, wangeendelea na dhambi zao. Basi nikaendelea kulia sana. Kisha akaniuliza kama nilikuwa nawafahamu wale watu, nikasema siwafahamu. Akasema twende huku, nikaendelea kukatiza katikati ya mabilioni ya watu waliofia katika dhambi, kila mmoja na uchungu wake na kila mmoja na mateso yake.
Mtu wa kwanza kumwona alikuwa babu yangu mzaa mama, yeye alikuwa ni mwinjilisti na mzee wa kanisawa kanisa la Lutherani, kule Isapulamo wilaya ya makete mkoa wa Iringa. Sasa nilishangaa sana kumuona katika sehemu hii ya Jehanamu, yeye akiwa duniani alikuwa mweupe sana. Lakini sasa nilishangaa kumwona akiwa mweusi kupita kawaida. Nikamwuliza, “mbona mtu huyu alikuwa mtumishi wa Mungu na sasa namuona sehemu hii?”  Yule Mtu akasema kweli kabisa huyu mtu alichaguliwa kwa ajili ya kazi ya Mungu lakini aliamua kuifanya kazi ya Mungu na kuingiza michanganyo ya dhambi. Na ndiyo maana unamuona sehemu hii, ulevi kidogo alikuwa nao, ushirikina kidogo na mambo mengine kama hayo, kama maandiko yasemavyo Ufalme wa Mungu wanauteka wenye nguvu tu. (Mathayo 11:12 na wagalatia 5:19-21)
Mtu wa pili alikuwa jirani yetu, alikuwa ni kaka mmoja aliyekuwa anasali kanisa la Moraviani. Alikuwa ni kaka mmoja aliyejipenda sana na kila siku ya ibada na Jumapili alishika Biblia na kitabu cha nyimbo na kwenda ibadani. Lakini kumbe alikuwa hayafanyi mapenzi ya Mungu (mathayo 7:21). Hata leo ukienda Uyole utasikia sifa zake. Huyu kaka alikuwa anaumwa sana na alilazwa katika hospital ya Mbeya, siku mbili kabla ya kufa kwake alituma watu kwenda kumwita mchungaji amwombee na baada ya siku mbili akafa. Sasa nikashangaa sana kumwona sehemu hii ya mateso, wakati huo huo watu wanasema mtu akiombewa anakwenda moja kwa moja mbinguni!  Yule mtu akaniambia kawaambie watu wote duniani, mtu yeyote aliyejua kuwa dhambi ni mbaya na kuwa itampeleka Jehanamu, akiendelea kutenda dhambi akisema nitatubu nikiona kwamba ninekaribia kufa, Mimi huyo simpokei (katika ufalme wangu).  Jinsi ninyi msivyopokea vitu vilivyooza ndivyo na mimi sivipokei japokuwa navitoa duniani (Ufunuo 22). Yule kaka akasema ninakuomba ukawaambie mama, baba na ndugu wasitende dhambi, i japokuwa mimi nimepata bahati mbaya kuja sehemu hii lakini kawaambie wasitende dhambi. Yule Mtu aliyekuwa ananiongoza akasema usiende kuwaambia kwa sababu duniani kuna wachungaji na waliookoka wanahubiri Injili, wasipowasikia hao, nyumba nzima watakuja huku (Luka 16:19-31)). Yule kaka akajitupa chini akalia kwa uchungu mkubwa mno.
Mtu wa tatu kunionyesha alikuwa mama yangu mdogo upande wa mume wangu. Mama huyu alikorofishana na wakwe zake (yaani wazazi wa mume wake) wakati mume wake alipokuwa amesafiri.  Basi akanywa vidonge vya sumu naye akafa; mume wake aliporudi na kuonyeswa kaburi la mkewe, naye akaamua kuchukua vidonge vya sumu na kunywa.  Sasa tulipokuwa tunaenda Kwa rafiki yetu kumwona (yule aliyempokea Yesu kama nilivyoeleza pale mwanzoni) ndipo tulipishana na gari lililokuwa linampeleka hospitali akiwa mahututi. Sasa nikashangaa sana kumwona katika ile sehemu ya mangojeo. Nikauliza huyu mtu nilimwacha duniani na sasa inakuwaje namwona huku?  Yule Mtu akasema, kawaambie ndugu zake duniani, mtu anapokufa duniani ile sekunde moja tu, huku amekuwa ameshiriki kiasi cha kutosha, kama ni mtu wa uzima (aliyekwenda mbinguni) amekuwa na Uzima, uzima tele na amekuwa mwenyeji, sasa huyu mtu hapa unavyomwona hata dakika kumi na tano hajamaliza. Nilishangaa sana maana alikuwa mweusi sana, ulimi wake umevutwa na kufika kifuani kama wale wengine. Alionekana kama vile mtu aliyekaa kwenye mateso yale zaidi ya miaka elfu kumi. Moyo wangu ulijaa huzuni na uchungu usio wa kawaida, basi yule mtu akaniambia sasa kawaambie watu wote jinsi ulivyoona, na jinsi ulivyosikia usiongeze wala usipunguze. Yule atakayekataa usimlazimishe wala kumbembeleza, atakayekubali umwelekeze jinsi ya kutubu na kuokoka.
Ndipo nikashangaa kwa ghafa kuwa nimetokea tena katika nyumba ya yule rafiki yetu, wenzangu wote wametulia wakisubiri litakalotokea, basi nikawaeleza yote niliyoyaona na kuyasikia nasi tukamshukuru Mungu kwa pamoja.
SURA YA 3
JERUSALEMU MPYA
Siku ya tarehe 31/12/1991 niliongozwa na Mama kwenda shambani. Nilimweleza habari zote za baba yake, lakini mama hakuwa na la kufanya zaidi ya kusikitika, kwa maana nafasi ya baba yake ina gharama wala haina budi kuiacha hata milele (Zaburi 49:7-8)
Baada kufika shambani tulianza kulima, nilichimba shimo la kwanza, la pili na tatu kwa ajili ya kupanda mahindi, mara nikaanza kujisikia vibaya, basi nikamwambia mama. Mama akasema mwanangu hivi sasa ni saa tatu asubuhi watu wakikuona unarudi nyumbani watashangaa sana, vumilia kidogo. Sasa sikumbuki kama niliongeza kuchimba shimo lingine au hapana. Nilishangaa niko kwenye sehemu nyingine ya tofauti kabisa na mazingira ya hapa duniani, sehemu hii ilikuwa inaleta matumaini sana.
Sehemu hii ilinivutia mno basi nikawaza moyoni kama asipotokea yule mtu wa jana nitang’ang’ania kubaki huku huku. Nikaamua kukaa mara nikasikia sauti nyuma yangu ikisema tufuate, nilipogeuka nikashangaa kuwaona Watu wawili waliofanana sana na Mtu wa jana katika hali zote. Mmoja ameshika upanga na alisema anaitwa Mikaeli na aliyekuwa ameshika karatasi alisema alisema anaitwa Gabriel. Wasomaji wa Biblia wanajua kazi zao (Danieli 10:13, Yuda 1:9 na Luka 1:26)
Nami nikasikia sauti ndani yangu ikiniambia, inua macho yako utazame mbele. Nilipoangalia nilishangaa sana kuona mbele yetu kulikuwa na nuru kubwa sana kutoka katika mji mmoja mkubwa na mzuri sana. Nuru ile iliangaza vizuri kuliko hata mwangaza wa jua na mwezi. Kwa kweli nilivutiwa sana na mji ule jinsi ulivyokuwa unapendeza. Nikauliza ule mji ni mji gani? Na ni kwa ajili ya nini? Wakaniambia Ule ni mji Mtakatifu, Yerusalem mpya na ni kwa ajili ya Watakatifu walioshinda ya mambo ya dunia. Kwa kweli nashindwa hata kuelezea uzuri wa mji ule maana hauna mfano wa aina yoyote hapa duniani. Tumani langu ni kwenda kuishi katika mji wa utukufu mwingi sijui mwenzangu unatumaini gani!
Tulipofika mlango wa lile jiji, mawazo yangu yalinipeleka moja kwa moja katika kitabu cha nyombo cha tenzi  za rohoni, namba 121, “Liko lango moja wazi”.  Niliona lango moja kubwa lililokuwa wazi, (Ufunuo 3:7-8) lango hili lilikuwa likibadilika kila aina ya rangi, nyingine hazipo duniani. Tulipoingia ndani karibu na mlango tulimwona mtu mmoja mzuri sana mweupe na aling’aa sana, alikuwa amekalia kiti kizuri na cha thamani sana, kupita kawaida.  Alionekana kuwa mtu mpole mwenye huruma sana na upendo (Mithali 11:28-30), tabasamu lake lilinipa raha ya aina yake na kunifanya nicheke sana kwa furaha na hata kujisahau. Malaika nilioongozana nao walianza kuzungumza na yule mtu kwa lugha nisiyoifahamu. Mimi nikaendelea kushangilia ule mji, ule mji umetengenezwa kwa vioo vitupu. Kila sehemu nilipotazama nilijiona mwenyewe (Ufunuo 21:18), nikaendelea kushangilia ule mji kwa uzuri wake na thamani yake hadi pale wale malaika waliponiambia kuwa niwafuate.
Malaika walinitembeza mji mzima kwa muda mfupi sana hata sekunde moja haikuisha, nilishangaa sana sijui wametembea vipi wale watu. Malaika wa Kwanza akafungua mlango akaingia wa kwanza, pili nikaingia. Katika sehemu hii niliviona viti vingi sana vilivyokuwa vimeandikwa majina kwa damu mbichi. Vile viti vilikuwa vizuri na vya thamani kupita kawaida. Nikaomba kukalia kiti kimoja nikaambiwa utakalia ukishinda mambo ya duniani.
Katika sehemu zote sikuona taa zikiangaza lakini kulikuwa na mwanga mzuri sana. Nikauliza mwanga huu unatokana na nini? Akaniambia mwanga huu ni wa Mwanakondoo uliyemkuta mlangoni.
Nilipoingia kila mahali nilipata mshangao sana na kustaajabia uzuri wa mji ule. Kila mlango ulibadili baina ya rangi, kisha tukaondoka sehemu hii. Akafungua mlango mwingine nikastaajabu kuona bustani nzuri sana iliyozungukwa na maua, (ya majani) na yote yalikuwa na urefu sawa bila kuzidiana. Tena yalikuwa ya kijani kibichi sana. Maua ya sehemu hii yalikuwa marefu na yanamsifu Mungu kupita kawaida, yakiinama upande wa kulia yanakwenda yote na kusujudu na kuinuka hutoa harufu nzuri sana inayoenea mji mzima, maua hayo yalikuwa yamezungukwa na kioo. Nikasema naomba nichume ua moja nikawaonyeshe ndugu zangu. Akasema maua ya huku hayachumwi, akasema bustani hii imetengenezwa kwa hajili ya utukufu wa Mungu, nilitamani sana kukaa sehemu hii ya bustani, lakini wakasema tufuate.
Kila mahali tulipokwenda mmoja akafuata mwingine, nikasikia sauti nzuri mno zikiimba kwa furaha sana, kasha tukaingia, nikashangaa sana kuona watu wengi sana wasio na idadi. Nikajiuliza kwa nini Mungu anasumbuka kuwatafuta wanadamu wakati anao wengi sana? Nikastaajabu sana, ndipo nikakumbuka wimbi mmoja unaosema; Ukiringaringa kwa Yesu, ana watu wengi.  Hawa watu walikuwa wanadamu kama sisi ambao waliishi duniani, lakini wao walimwishia Mungu na kufa katika utakatifu.
Kama umewahi kuona mapacha basi wale ni mapacha wa aina yake. Sura zao hazitofautiani hata kidogo wamefanana sana isivyo kawaida. Nywele zao zilikuwa ndefu wamezibana kwa banio jekundu sana, wala si wembamba sana na nilifanikiwa kugundua tofauti moja tu. Wengine wamevaa mikanda miwili kiunoni na wengine mkanda mmoja. Nikauliza kuna tofauti gani kati ya waliovaa mkanda mmoja na waliovaa mikanda miwili! Akasema waliovaa mmoja ni wanaume na waliovaa miwili ni wanawake. Lakini ilikuwa sio rahisi kuwatofautisha kuwa huyu ametoka taifa hili na yule taifa lingine, waliimba wimbo mzuri isivyo kawaida, staili za uimbaji wao kwa kweli zilinifurahisha mno walipunga mikono yao wote kwa pamoja na hapakuwepo hata mmoja wao aliyekosea.
Nilipozidi kuwatazama nilitamani sana kujiunga nao ili nami niimbe na kumsifu Mungu kama wao wanavyosifu, lakini haikuwezekana kwa sababu hata lugha yao nilikuwa siijui. Baada ya muda akatokea dada mmoja, naye akuja upande wangu, niliweza kujua ni mwanamke kwa sababu alikuwa na mikanda miwili, nilishangaa kumuona yule dada kwa sababu niliweza kumtambua, hii ni baada ya sura yake ile ya duniani kutokea. Yeye alikufa mwaka 1987 mwezi wa nne na aliuawa kwa kupigwa risasi. Yeye alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mbeya (Mbeya Day secondary school), alifariki akiwa kidato cha tatu (Form Three). Aliponifikia alisema, Ah Nyisaki! “Umekuja huku” nikasema Ndiyo. Akasema za duniani, nikasema Duniani matatizo, akasema ni kweli ni matatizo.  Angalia wenzenu tumevikwa miili mipya isiyoharibika, isiyopata magonjwa, yaani aliusifu mwili wake na ni kweli ndivyo alivyokuwa, soma (1Korintho 15:40-53).
Akasema mwili wa zamani tumeuacha pale, basi nikageuka niangalie anaponielekeza ni wapi! Kweli ndugu yangu Biblia inasema mtafuteni Bwana maadamu anapatikana, mwiteni maadamu ya karibu (Isaya 55:6-7).  Ndipo nilipotazama, mambo yote ya Uyole, mkoani mbeya niliweza kuyaona kama vile unavyoweza kutazama kitu kwenye kiganja chako cha mkono. Nilipoangalia sokoni nikaona biashara zinaendelea kama kawaida, barabarani magari na baiskeli ziliendelea kupishana kama kawaida, nilipotazama makaburini mahali aliponionyesha huyu Dada, nikaona makaburi ya watu wengi tena niliweza hata kusoma majina yao. Pia niliweza kujua wazi kabisa kuwa huyu yupo uzimani au jehanamu. Na kama hayupo ilionyesha wazi yuko uzimani. Kaburi la huyu dada lilionekana pia, likiwa limepambwa maua. Akasema umekiona kile kitu?  Nikasema ndiyo, akasema Ule ndio mwili wako.
Kwa kweli sikupenda kuutazama mwili ule mara mbili, mwili wangu niliuona kama ngozi ya kenge, chafu sana akaniambia geuka tena, nikakataa, mara ya pili nikakataa, mara ya tatu nikageuka, nami nikaona kama mtu analima na kupanda mbegu shambani, yule Mtu akasema yule ni mama yako, fahamu zake tunazo huku, atarudishiwa fahamu zake wewe utakaporudi duniani. Maono ya siku hiyo yalikuwa ya muda mrefu, kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni. Nilipochukuliwa kwenye maono haya,  mama aliubeba mwili wangu  na kuuweka kivulini, hapo ndipo nilitambua kweli fahamu zake zilichukuliwa. Yule dada akasema Nyisaki kawaambie ndugu zangu wasitende dhambi tena, katika mji huu hakuna huzuni wala shida, lakini bado ninawaona wanaendelea kutenda dhambi, ninasikitika sana.  Wale Malaika wakasema, usiende kuwaambia kwa sababu kule kuna waliookoka ambao wanahubiri Injili na habari za wokovu, wasipowasikia hao basi hawataingia katika mji huu.
Mtu wa pili kunionyesha alikuwa mzee mmoja wa makamo, ambaye aliyedharauliwa sana pale Uyole. Alidharauliwa kwa sababu yeye alikuwa rafiki saa wa  Biblia na kitabu cha nyimbo cha Tenzi za Rohoni,  na kila alipojipumzisha iwe ni shambani, nyumbani au sehemu nyingine yoyote alisoma Biblia, aliimba Tenzi na kumwomba Mungu.Kwa kweli yule mzee alijishusha sana mbele za Mungu (Luka 14:35, 18:17, Isaya 51:7-8) watu wengine walisema kuwa amechanganyikiwa. Nilishangaa kumuona katika sehemu hii akiwa kama kijana wa miaka ishirini (20), naye pia aliusifu mwili wake isivyo kawaida, kweli miili ile ni mizuri sana. Akasema kawaambie wapendwa wa duniani kila mmoja ajitahidi ili ayashinde mambo ya duniani maana muda umeisha (Ufunuo 22:10-14). Kila mmoja aangalie sana shetani asimpumbaze (na kumdanganya hata akayapenda mambo ya duniani na dhambi).  Sisi tuna hamu kubwa kuwaona wapendwa wetu, ndipo akaondoka na kuchanganyikana na wenzake.
Baada ya hapo akatokea mtu wa tatu, naye nilimtambua kuwa ni mwanaume kwa sababu ya ule mkanda mmoja, aliponikaribia ndipo ikatokea sura yake ya duniani. Yeye alikuwa mzee wa kanisa la Pentekoste, alikuwa anaabudu Kanisa la Assemblies of God, naye akasema, Ah Chaula umekuja huku nikasema Ndiyo,  akaniambia za duniani? Duniani matatizo, akasema Kweli matatizo, angalieni wenzenu tumevikwa miili mipya isiyosikia njaa, isiyopata magonjwa. Basi aliusifu ule mwili, kweli alikuwa amebadilika naye alionekana kama kijana wa miaka ishirini (20) hivi. Baada ya hapo akaondoka na akaendelea kuimba. Baada ya kuonana na hao watu nikawauliza hao Malaika, hivi hawa watu wanajifunza kuimba? Wakasema kwa nini unasema hivyo, nikasema wanaimba wimbo na hauishi. Akasema huku sivyo kama mnavyoimba duniani, maana duniani mkiimba dakika tano mnasema tumemsifu sana Mungu na wengine wanadhani watakwenda mbinguni kwa sababu ya uimbaji bila kuokoka. Wimbo mmoja wa huku unaimbwa kwa miezi tisa, beti moja miezi mitatu, Chorus inaimbwa miezi mitatu na beti ya mwisho miezi mitatu, basi nikashangaa sana. Tukaondoka hii sehemu akasema twende nikakuonyeshe watakatifu waliokuwako wa mwanzo wa kanisa, maana wameletwa sehemu yao.  Akafungua mlango, tukaingia, ndipo nikaonyeshwa watu kumi na sita (16), lakini nilijua wazi walikuwako na wengine zaidi.
Mtu wa kwanza alikuwa Bartholomayo, naye akanikumbatia na kunishika mkono, akasema huyu ndiye aliyechunwa ngozi kwa sababu ya Injili. Na mtu wa pili kunionyesha alikuwa ni Yohana Mbatizaji, nikasema ndiye aliyekatwa kichwa kwa sababu ya Injili, akasema ndiye huyu. Basi akanikumbatia na kunishika mkono (soma Mathayo 14:1-11). Mtu wa tatu kunionyesha alikuwa ni Eliya, Mtaabishaji wa Israel (1Wafalme 18:17-18), naye akanikumbatia na kunishika mkono. Malaika alinionyesha watakatifu wengi sana, akina Paulo, Petro na Yohana na wengineo. Batholomayo akasema, Mpendwa, kawaambie wapendwa duniani, wakaze mwendo maana sekunde moja siyo muda mrefu (Filipi 3:12, 1Korintho 9:24-27), ndipo tukaondoka ile sehemu.
Wakanipeleka sehemu ambayo zinaandaliwa nguo za kuvaa watakatifu katika karamu ya Mwanakondoo, katika sehemu ile niliwakuta malaika wengi mno wakimsifu Mungu kwa shangwe. Katika sehemu hii pia kulikuwa na mashine nzuri zilizotengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu mno, nguo nyingi sana ziliingia ndani ya mashine na kutolewa zikiwa zinang’aa sana, nikauliza mbona nguo nyingi sana zinatengenezwa, ni za nani? Maana watu wengi wanaukataa Wokovu duniani. Akasema, Ninyi kaihubirini injili tu, anayetaka kuokoka na aokoke asiyetaka akatae, kinachotakiwa ni kwamba anapokuja Mwana wa Adamu asiwepo wa kusema mimi sikusikia.
Basi tukaondoka ile sehemu. Ule mji ni sifa kila kinachofanyika, kilifanyika huku wakimsifu Mungu, si malaika wala si mwanadamu, si maua, si vinanda, maana vinanda vya kule vinapiga vyenyewe. Wakanipeleka katika ile sehemu ya awali iliyokuwa na viti vingi vyenye majina yaliyoandikwa kwa damu mbichi.
Tulipofika mara ya kwanza hakukuwa na mtu, lakini muda huu tulimkuta Mtu mmoja aliyekuwa akifanya kazi kwa haraka sana, alikuwa amekazana sana kuliko hata roboti (alifanya kazi hiyo kwa upesi mno). Nilimwuliza katika mji huu kuna watu wawili Kama hawa!?  Tena kwa nini wamekazana sana namna hii. Akasema Mtu huyu ni mmoja, kumbuka maneno yake alipokuwa anaondoka duniani alisema, “Ninakwenda kuwaandalia mahali ili alipo nanyi pia muwepo” (soma Yohana 14:1-6). Akasema huu mji ameuandaa mwenyewe hakuna mtu aliyemsaidia. Tena amekazana kwa sababu muda umefika wa kuwachukua watu walio wake duniani (soma  1Thesalonike 4:13-17).
Wakaniondoa sehemu hii. Sehemu inayofuata ambayo nilipelekwa, ni sehemu muhimu sana, umesoma na kusikia habari zote za kwanza, sasa naomba utulie na kusoma vizuri.
SURA YA 4
MANGOJEOYA WAFU NA JEHANAMU YA PILI
Mmojawa wale malaika akaniambia sasa tunakwenda kukuonyesha Jehanamu – sehemu ya pili. Mimi nikasema, Ah!  Kuna sehemu nyingine tena! Akasema, Ndiyo, hii imezidishwa ukali mara saba zaidi (soma Mithali 15:10).
Baada ya mazungumzo hayo, ndani yangu furaha ya uzima wa milele ikatoweka, nikawaza ikiwa sehemu ile ya kwanza nililia vile, Je sehemu ya pili hii itakuwaje? Nikawafuata katika sehemu hii ya mangojeo. Sehemu hiyo  peke yake ilinitoa raha, kwa sababu ilikuwa ni kama mara saba zaidi ya ile ya kwanza. Watu wake walitoa sauti za uchungu mkubwa mara saba zaidi, watu niliowaona ni wale wote waliozijua siri za Mungu na kuzidharau, ni wale wote waliookoka na kasha wakaacha wokovu (soma Ebrania 2:3, 6:4-6). Ni mchungaji na waalimu (Yakobo 3:1, Ezekieli 34:2-6) wanalia milele na milele bila kutoa hata chozi moja. Kabla hata ya kuonyeshwa nililia kwa uchungu sana na kuishiwa nguvu mwilini.
Akainuka mtu wa kwanza (aliyekuwa kwenye mateso) akasema, Bwana naomba umtume mtumishi wako aniletee tone la maji niuburudishe ulimi wangu. Mpendwa hebu jiulize wewe upo duniani, je unaridhika na tone moja la maji! Basi sehemu ile tone moja la maji lina thamani sana wanalilia tone hilo usiku na mchana!
Malaika akawaambia mlipokuwa duniani mliichezea neema ya Mungu, sasa hii ni sehemu ndogo sana ya mateso bado sehemu yenyewe ya hukumu. Yule mtu akajitupa na kuendelea kulia kwa uchungu mno nilimwangalia tena, naye haikuinuka kabisa.
Nikaendelea kuwafuata wale watu huku nikilia na kutembea kwa taabu mno, tukamkuta mtu wa pili naye akasema, Bwana utupe sekunde kumi (10) tukaihubiri injili ulimwenguni ili wanadamu waokoke. Yule Malaika akasema mlipokuwa duniani mlikuwa na muda mwingi sana wa kuihubiri injili lakini mliutumia kwa tamaa zenu, sasa hii ni sehemu ndogo tu ya mateso. Nikalia kwa uchungu sana. Hakuinuka tena, mateso waliyonayo yanawafanya waombe sekunde kumi (10) kuhubiri.
Mpendwa, muda uliupoteza kwa mambo yasiyo ya maana utadaiwa na Mungu, maana kama wewe ungehubiri injili ipasavyo, Jehanamu ingekosa watu wa kwenda kwa sababu ungekuwa umeutumia vizuri muda wako kuhubiri injili kila mahali.
Mara nikasikia kigelegele cha kutisha mno, nikauliza hivi, Je kuna mtu ametupwa motoni? Wakasema hapana. Tumesema jehanamu hii imezidishiwa ukali mara saba zaidi. Sasa kigelegele hicho ni cha moto, kikishangilia kwa sababu muda wake umefika. Nikasikia mara nyingine tena, nikauliza vilevile nikaambiwa mbona wewe husikii, jehanamu hii imezidishwa mara saba zaidi. Wale watu wanasikia vigelegele vya kutisha lakini hawana la kufanya zaidi ya kusubiri mateso, tofauti na duniani ambapo mtu akipata shida kidogo anajiua, lakini sehemu hii haiepukiki ama kutoroka. Tofauti nyingine tena ni kwamba duniani mtu anayo nafasi ya kutubu na Kumwani yesu Kristo, lakini sehemu hii hakuna nafasi hyo.
Ndani ya ule moto niliwaona Funza waliokonda sana, basi nikasikia sauti kutoka upande ule ikisema Bwana watu uliosema utawaleta watakuja lini?  Nikashituka na kuuliza je huku kuna mtu, funza hao waliongea lugha ya Kiswahili. Akawaambia wale funza, subirini kidogo, hapo ndipo walipoonekana kuwa wamechokozwa. Hakukuwa na maelewano kabisa, walipiga kelele wakisema chakula chetu.
Akaniambia hao funza kama ulivyowaona wamekonda, watakapomshika mwanadamu ipo kazi (yaani watamtesa sana). Nililia sana hadi wale malaika wakaamua kuniondoa sehemu ile. Akasema sasa, nenda kawaambie watu wote duniani, usiongeze wala usipunguze lolote. Nikasema Bwana Mimi duniani siendi wala hapa sikai, naomba mnipeleke kwa wale wanaoimba na kusifu. Basi akanigusa bega langu, nikashangaa nimetokea shambani kwetu, na ilikuwa saa kumi na mbili jioni. Ndipo mama aliposhtuka na kuja kuniona pale aliponilaza.
Sasa ndugu yangu, nimekueleza jinsi ilivyokuwa na sasa ni juu yako wewe kufanya uamuzi, kuwa utubu dhambi zako na kumfuata Yesu Kristo au ukatae habari hizi, maamuzi ni yako. Umekwisha sikia yote, Mimi sijaongeza wala sijapunguza neno lolote kama nilivyoagizwa (Mathayo 7:13-14, Kumbukumbu 3:19-20).
MIMI SITAONGEZA NA SASA NI KAZI KWAKO KUAMUA (Ufunuo 3:20)!
MUNGU NA AKUBARIKI
Mwisho kunukuu yale yaliyoandikwa na kushuhudiwa na mtumishi wa Mungu, Nyiska Chaula.
UNACHOTAKIWA KUFANYA
Upendo wa Mungu kwa Mwanadamu ni mkubwa sana, ndio maana alimtoa mwanawe pekee Yesu Kristo kwa ajili ya dhambi za wanadamu (soma yohana 3:16). Mungu hataki mtu yeyote apotee na kuangamia katika dhambi (soma yohana6:39-40), bali watu wote waokolewe kwa njia ya Kumwamini Yesu Kristo. Biblia inasema, “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi( Yesu Kristo) nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele” (yohana 10:10)
Huu ndio wakati wa kumgeukia Mungu na kufanya yaliyo mapenzi yake. Ikiwa tayari mekwisha kumpokea na kumwamini Bwana Yesu Kristo umefanya uamuzi wa busara. Biblia inasema, “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao” (waebrania 12:14). Pia mathayo 5:8 inasema, “Heri wenye moyo Safi; Maana hao watamwona Mungu”. Mistari hii inatufundisha kuwa ili kuurithi uzima wa milele mbinguni, tunatakiwa kuishi maisha matakatifu mbele za Mungu, yaani kufanya yale yanayompendeza. Kuwa mkristo na kuifanya kazi ya Mungu kama kuhubiri, kuimba, kutoa sadaka n.k haviwezi kutuingiza mbinguni (soma mathayo 7:19-21). Inatupasa kuishi maisha safi, yasiyo na dhambi.
Hii inawezekana kwa sisi kumtegemea Roho mtakatifu na kuwa karibu naye, yeye ndiye msaidizi wetu (yohana 14:26). Pia ni muhimu kulisoma Neno la Mungu kila siku, kuliamini mioyoni mwetu na kulitenda kila siku. Pia inatupasa kudumu katika maombi, na kuzidi kuwaombea wakristo wote na pia kuwaombea watu ambao bado hawamjua Yesu Kristo kama mwokozi wao. Mtume Paulo anasema, “Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele;  nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.” (wafilipi 3:13-14). Ewe mwana wa Mungu, uliyeokolewa na Kristo Yesu, kaza mwendo, ukaishinde dhambi na mambo yote ya dunia ili ukaurithi uzima wa milele mbinguni!
Ikiwa haujampokea Yesu Kristo kama mwokozi wako, basi leo ndiyo siku ya kufanya uamuzi huo  muhimu. Unaweza kufanya sala ifuatayo, na Yesu Kristo atakusamehe makosa yako na kuingia ndani mwako. Ifanye kwa moyo, ukiamini kuwa Mungu anakusikia! Sema maneno haya;-
        Ee Bwana Yesu, ninakuja mbele zako, mimi ni mwenye dhambi na mkosaji. Asante kwa kuwa ulijitoa, ukafa kwa ajili ya dhambi zangu. Ninatubu mbele zako, ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizozifanya,  ninaomba unioshe moyo wangu na kunitakasa kwa damu yako ya thamani. Ee Yesu, ninakukaribisha moyoni mwangu, uwe Bwana na mwokozi wangu tangu sasa na hata milele. Asante Bwana Yesu kwa kunisamehe dhambi zangu, kuigia ndani mwangu na kunipa uzima wa milele. Ninaomba unisaidie Mimi, Ili nidumu Na kukua ndani yako siku zote, majaribu yasinishinde, dhambi zisinishinde, shetani asinishinde Na dunia hii isinishinde, kwa jina la Yesu ninaomba. Amen.
Ikiwa umefanya na kuikiri sala hiyo, basi amini na ujue kuwa Yesu Kristo amekusamehe dhambi zote na kukupa Wokovu. Inakupasa kudumu ndani mwake na kuwa na ushirika na yesu Kristo, hii ni kwa kulisoma neno lake kila siku (katika Biblia) na kuzungumza naye kwa njia ya maombi.
Pia ni muhimu utafute kanisa au kutanika la watu wanaompenda na kumwamini Yesu, jumuika nao ili uweze kukua na kuzidi kumjua Yesu Kristo.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

KUISHI MAISHA YA UTAKATIFU.

Utakatifu  - Ni maisha ya Mkristo anayoyaishi kwa kuzingatia kanuni ya neno la Mungu baada ya kumkiri na kumpokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake. Kuishi maisha ya utakatifu ni jambo linalowezekana, kwa sababu Mungu alipomuumba mwanadamu alimwekea hiari ndani yake kwa kutokea kwa tukio. Ndio maana Yesu alipokuwa akifundisha alitumia mfano wa mti kuonyesha mtu anavyoweza kuishi maisha haya ya kumpendeza Mungu au ya maisha ya dhambi. "   "Ufanye mti kuwa mzuri na matunda yake kuwa mazuri, au ufanye mti kuwa mbaya na matunda yake mabaya, kwa maana kwa matunda yake mti hutambulikana" Mathayo 12:33. Kuishi maisha ya utakatifu ni agizo la Mungu kwa wale wote aliowachagua. Ndio maana Mungu alimwambia Musa,   "Nena na makutano wote na wana wa Israel, uwaambie, mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana Mungu wenu ni mtakatifu"  Walawi    19:2. Kuwa mtakatifu ni kumpendeza Mungu, kwa sababu amesema;  “Watakatifu waliopo duniani ndio walio bora...

KUMTUMIKIA MUNGU KWA BIDII.

Kutokana na kichwa cha somo hapa juu katika matukio wazi ili mtu amtumikie Mungu ni lazima awe na bidii. Kwa sababu hiyo kwa mtu yule ambaye ameweka nia moyoni mwake ya kwamba atatumikia Mungu kwa bidii. Tukiangalia kuhusu mwanadamu kuna mambo mengi katika maisha yake ameyafanya kutokana na bidii aliyo nayo. Lakini ikiwa mtu hana bidii kwa ajili ya mambo ya Mungu kamwe hawezi kuingia ufalme wa Mungu. Ndio maana imeandikwa;  "Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatimkana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka,   Mathayo 11:12 ."    " Torati na manabii vilikuwapo mpaka Yohana; tangu wakati huo habari njema ya ufalme wa Mungu hutangazwa, na kila mtu hujiingiza kwa nguvu."   Luka 16:16. Hapa ninatoa ushuhuda wangu binafsi, kuhusu kumtumikia Mungu kwa bidii. Wakati nilipookoka nilikuwa na kiu au shauku kwa ajili ya kutaka kujazwa Roho Mtakatifu. Kwa sababu nilikuwa ninamhitaji sana nilimwomba mtumishi mmoja wa Mungu aniombee ili niweze kujazwa...

TUNDA LA UAMINIFU.

Uaminifu ni mojawapo ya tunda la Roho katika maandiko matakatifu. Tutajifunza uaminifu wa Mungu unaopatikana katika neno lake. Yeye amesema atatimiza yale aliyoahidi katika neno lake, si tu kwa wana wa Israel bali kwa watu    wote wanaoishi sawasawa na neno lake. Kwa hiyo, kwa upande wetu inatupasa sisi nasi kuwa waaminifu kwa kuliishi na kulitenda neno la Mungu.   “Basi jueni ya kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye Mungu; Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake, hata vizazi elfu.   Na itakuwa, kwa sababu mwazisikiza hukumu hizi, na kuzishika na kuzitenda, basi Bwana, Mungu wako, atakutimizia agano na rehema aliyowaapia baba zako.”   Kum 7:9, 12.   “Ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu    halitanirudia bure bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.   Isa 55:11" Tabia ya mtu mwaminifu. 1. Mtu aliye mwaminifu ni yule ambaye anatenda sawa...

UPONYAJI WA MAGONJWA.

Chanzo cha magonjwa. Kuna magonjwa yanayotokana na mtu kufanya dhambi. Ndiyo maana Yesu alipomponya yule mtu ambaye aliyekuwa mngonjwa akamwabia,   “…Angalia umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi”   Yn 5:14.   Ikiwa mtu aliyeokoka akirudia kuishi maisha ya dhambi pepo mchafu anapoona nafasi anachukua pepo wengine na kuingia kwake. Yesu alisema,  “Mara huenda akachukua pamoja naye    pepo    wengine walio waovu    kuliko yeye mwenyewe nao huingia na kukaa humo; na mtu Yule hali yake huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya”   Mt 12:45.    Wakati mwingine sii kila mtu anayeumwa amefanya dhambi, bali ni matokeo ya ugonjwa katika mwili. Kwa upande mwingine mtu anaweza akawa ni mgonjwa au amekosa lishe.  Uponyaji wa Mungu.                     Mambo ya kuzingatia na kuponywa ni ha...

KUWEKWA HURU KUTOKA DHAMBI YA UZINZI NA UASHARATI.

Jambo la kwanza ninamshukuru Mungu kwa neema yake aliyonipa kufundisha neno lake. Ndungu mpendwa ninajua ya kwamba Mungu alikupenda sana, hata akamtoa Mwana wake wa pekee Yesu Kristo kwa ajili yako ili akukomboe kutoka katika dhambi zote ikiwemo dhambi ya uzinzi na uasherati. Sasa ninakusihi kwa neema ya Mungu fuatana nami kwa makini kuhusu  somo hili nawe utauna utukufu wa Mungu katika maisha yako. Tunaweza kuangalia kwa makini dhambi ya uzinzi na uasharati ambayo mtu akiitenda inaharibu ufahamu wake na hatimaye kuangamia. Mtu anapoteza uhusiano wake na Mungu, mawasiliano kati yake na Mungu yanakatika. Mungu  ni Makatifu hana ushirika na wenye dhambi. “Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake.” Mithali 6:26.   “Lakini maovu yenu yamewafarikisha (yamewatenganisha) ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki  kusikia.”   Isahau 59:2. Atendaye dhambi ya zinaa au  uasherati ...

KUDUMU KATIKA UPENDO WA MUNGU.

Neno la Mungu katika Biblia linatufudisha kuhusu upendo wa Mungu  kwetu. Yeye Mungu ndiye  mwanzo wa upendo kwa sababu alitupenda kwanza. “...alitupenda sisi kwanza”.   1 Yohana 4:19. Jinsi mtu anavyoweza kuwa na upendo wa Mungu. Ni pale mtu anapokuwa amezingatia kudumu katika upendo wa Mungu kama ifuatavyo; 1.Kuishi sawasawa na maagizo yote ya neno la Mungu na kumpenda. “Na sasa, Israeli, BWANA, Mungu wako, anataka nini kwako, ila umche BWANA, Mungu wako, na kwenda katika njia zake zote, na kumpenda, na kumtumikia BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote;”   Kumbukumbu la Torati 10:12.   “Lakini mjibidiishe sana kuzifanya amri na sheria, ambazo Musa, mtumishi wa BWANA, aliwaamuru, kumpenda BWANA, Mungu wenu, na kwenenda katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na kushikamana na yeye, na kumtumikia kwa moyo wenu wote na nafsi yenu yote”.   Yoshua 22:5. 2. Jambo lingine la kuzingatia ni kwamba yampasa mtu kuyashika maagiz...

MADHARA YA DHAMBI.

Huu ni wakati mwingine ambao Bwana amenijalia kuwepo kwa kusudi lake jema. Nitaelezea katika somo hili kuhusu dhambi ilivyo na madhara kwa mtu aitendaye. Kwanza tuangalie dhambi  ilivyoanza kwa Adamu na Hawa ni wakati walipokula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya ambayo Mungu aliwakataza wasile. Kwa sababu hiyo dhambi ilisababisha madhara mengi kwa uzao wake na vizazi vyote duniani. Kwa hiyo shida zote zilizopo duniani zimetokana na dhambi. Kutokana na wazazi wetu wa kwanza Adamu na Hawa kwa kuwa walitenda dhambi na vizazi vingine vyote vimehesabiwa ni wenye dhambi. Mtu  anazaliwa akiwa na asili ya dhambi kutoka kwa wazazi wa kwanza Adamu na Hawa. Warumi 3:23 “kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;” Kutokana na sababu hiyo ndio maana kila mwanadamu anakufa sawasawa na Mungu  alivyosema katika kitabu cha Mwanzo 2:16-17 “BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa u...