Kuomba kwa nidhamu ni jambo jema. Ikiwa mtu haombi kwa busara anakuwa anakera na kuwaudhi watu wengine. Nimekuwa nikiona baadhi yao waliookoka wanapokuwa katika ibada wanafanya mambo ambayo si kwa kutumia busara. Ni haya yafuatayo:
1. Kuomba kwa kupaza sauti na kulia. Kufanya hivyo ni jambo jema ikiwa kanisa lina jambo zito ambalo wamepatana kuliombea. Lakini ukiwa na jambo lako lolote hata kama ni zito omba kwa sauti ya kawaida na kulia kmya kimya. Wala usikunje uso wako. Tuaweza kujifunza kwa Hana alivyoomba kwa busara katika hekalu. Ijapokuwa alikuwa na jambo gumu hakupaza sauti na kulia. “Ikawa, hapo alipodumu kuomba mbele za BWANA, Eli akamwangalia kinywa chake. Basi Hana alikuwa akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe; kwa hiyo huyo Eli alimdhania kuwa amelewa.” 1 Samweli 1:12-13
2. Kuomba kwa kukunja uso. Kwa kufanya hivyo unakuwa umeharibu muonekano wa uso wako. “Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao.” Mathayo 6:16
3. Kuomba kwa kutumia nguvu kwa njia ya kurusha rusha mikono. Kwa kufanya hivyo si sahihi kwa sababu kumwomba Mungu ni katika Roho mtakatifu, wala si kwa kutumia nguvu za mwili. “kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;.” Waefeso 6:18
Ndugu wapendwa katika Bwana tunaweza kuona mambo hayo kama ni ya kawaida, lakini yanaharibu heshima na hadhi ya kanisa la Mungu. Nasema hivyo kwa sababu wale ambao bado hajafahamu habari njema ya wokovu wataona tunafanya vitendo vya hovyo. Kwa sababu hiyo hawataelewa wokovu ni njia nzuri ya ufalme wa Mungu.
Hivi sasa kanisa ambalo ni mimi na wewe yatupasa kuwa makini katika hekima ya Mungu na kufahamu ni jambo lipi linafaa kwa wakati gani. Pia kutambua ni jambo lipi lisilofaa na kuliacha. Ninawatakia neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi Amina.
Maoni
Chapisha Maoni