Kutokana na kichwa cha somo hapa juu ni kweli mwanadamu hufanya dhambi kwa hiari. Nasema hivyo kwa sababu Mungu alimuumba mtu na kuweka ndani yake utashi wa kufanya maamuzi katika mambo mbalimbali. Lakini sii kila jambo ambalo mwanadamu alifanyalo ni sawasawa na neno la Mungu. Ijapokuwa Mungu ametuwekea hiari ndani yetu sii kwa ajili kuamua kutenda mabaya, bali ni kwa ajili ya kutenda mema sawasawa na neno lake.
Ni muhimu kufahamu ya kwamba kusudi la Mungu kumuumba mwanadamu ni ili aishi kama neno lake linavyosema. Ndio maana neno la Mungu linasema katika waefeso, “Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.” Waefeso 2:10. Pia Yesu wakati akifundisha alidhihirisha wazi ya kwamba mtu anaweza kufanya mema au mabaya. Kwa sababu hiyo anaonesha ya kwamba mwanadamu anayo hiari ya kuamua katika mambo ya Mungu. “Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake kuwa mazuri; au ufanyeni mti kuwa mbaya na matunda yake mabaya, kwa maana kwa matunda yake mti hutambulikana.” Mathayo 12:33. “Angalieni, nawawekea mbele yenu hivi leo baraka na laana; baraka ni hapo mtakapoyasikiza maagizo ya BWANA, Mungu wenu, niwaagizayo leo; na laana ni hapo msiposikiza maagizo ya BWANA, Mungu wenu, mkikengeuka katika njia niwaagizayo leo, kwa kuandama miungu mingine msiyoijua.” Kumbukumbu la Torati 11:26-28.
Kwa kuwa mwanadamu anayo hiari na maamuzi shetani hana mamlaka juu yake kumlazimisha kufanya dhambi. Ninasema hivyo kwa sababu shetani kazi yake yeye ni kujaribu mtu na kumshawishi ili afanye dhambi. Kuna njia ambazo mtu anaweza kujaribiwa ni kama ifuatavyo;
1. Tunaweza kuona njia ya kwanza ambayo mtu anaweza kujaribiwa ni kupitia Shetani. Hawa alijaribiwa na Shetani naye aliposhawishika alikula matunda aliyokatazwa na Mungu asile. Alikuwa amedanganywa na Shetani ili amkosee Mungu. “BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.” Mwanzo 2:16-17. “Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa.” Mwanzo 3:4.
2. Mtu hujaribiwa mwenyewe kwa yale anayoyatamani. Hapa nitatoa mifano ili uweze kuelewa. Ikiwa kuna mtu anatamani kuwa na gari, nyumba ya kisasa, simu ya mkononi. Lakini hana fedha za kununulia vitu hivyo. Kwa sababu ya tamaa zake akashawishika moyoni mwake na kuamua kuvipata kwa njia za wizi, dhuluma, na unyang’anyi, anakuwa amejaribiwa na tamaa zake mwenyewe. “Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa.” Yakobo 1:14.
3. Pia mtu apotamani kufanya mambo yoyote ambayo ni kinyume na neno la Mungu Shetani anaweza kumwingia na kumshawishi ili afanye haraka na kumkosea Mungu. Tuaweza kuona alivyofanya kwa Yuda Iskariote. “Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara. Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao.” Luka 22:3-4.
Kutokana na somo hili unaweza kuona wazi ya kwamba Shetani hahusiki kwa kila jambo. Kwa sababu hiyo kuna mambo ambayo Mwanadamu anafanya kwa Upumbavu na uzembe, hapa Shetani hahusiki. Kuendelea kujifunza zaidi bofya hapa; Kuepuka dhambi.
Maoni
Chapisha Maoni