Mkristo ambaye ameokoka anapaswa kuwa na imani iliyo kamili.
Mtu huyo anaweza kuwa na imani kamili iwapo atazingatia na kuzitenda
sheria zote za Mungu. Jambo hili ni la muhimu kwa kila mtu anayetarajia
kuurithi ufalme wa Mungu. Iwapo mtu atakuwa anatenda baadhi ya sheria za
Mungu na kuziacha nyingine huyo atakuwa amefanya au kuenenda kinyume na
imani ya neno la Mungu. Kwa maana hiyo mtu wa namna hiyo hataweza
kuurithi ufalme wa Mungu.Yafuatayo ni mwendelezo wa mambo
muhimu ya kuzingatia na kuyafanya ili mtu aweze kuwa na
imani iliyo kamili mbele za Mungu;
1. Kudumu katika kutenda sawasawa na neno la Mungu.
2. Kila jambo lolote unalolitenda ni lazima
kuhakikisha liko sawasawa na neno la Mungu.
3. Kudumu katika kuomba kila siku.
Mtu anayezingatia kuomba humshinda yule adui na hila zake zote.
Jambo hili ni muhimu tunaweza kujifunza kutoka kwa Bwana wetu Yesu
Kristo na mitume wake walivyoomba kwa bidii kila siku. Wao ni
kielelezo kwetu kwa sababu walidumu katika kuomba na pia waliweza kumshinda
shetani na majaribu yake yote.
Kama mtu hazingatii kumwomba Mungu kila siku inakuwa ni mwanzo wa yeye kuanza kupoteza uhusiano wake na Mungu. Mtu wa namna hiyo hawezi kusimama imara na kuishi sawasawa na neno la Mungu linavyosema. Kwa sababu hiyo ni rahisi kutenda dhambi anapojaribiwa na yule mwovu. Ndio maana Yesu aliwaagiza wale wanafunzi na kuwaambia; "Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu". Mathayo 26:41.
4. Kuutawala moyo wako na usiruhusu mawazo mabaya.
Hili ni jambo linalowezekana iwapo utaamua na kuweka nia ya kwamba
hutawaza mawazo mabaya.
5. Kutawala kinywa chako usinene maovu, maneno
yasiyofaa, maneno ya hovyo ya mitaani na ya utani (mzaha/masihara). Ikiwa
mtu atasemezana na mtu mwingine kwa utani kwa kufanya hivyo atakuwa
amesema uongo.
6. Kuzungumza kwa kiasi.
Usiwe mwepesi kuongea kupita kiasi kwa sababu kwa kufanya hivyo
unaweza kumkosea Mungu. Ni jambo la muhimu kufahamu ya kwamba kabla ya
kusema au kujibu neno lolote, yakupasa kwanza kufikiria ili uweze
kujua jinsi ikupasavyo kusema. Hapa ninasema hivyo kwa sababu
katika kunena kuna mtego wa kujikwaa. Dhambi ya namna hii baadhi ya
watu wengi wanaifanya. Dhambi nyingine ambayo watu wengi
wanaifanya ni kusema uongo kwa kusudi la kuficha mambo fulani
ambayo hawataki yafahamike kwa watu wengine.
7. Kuutawala mwili wako na kujilinda ili usije ukafanya dhambi ya
uzinzi na uasherati. Jambo hii linawezekana ikiwa mtu ataepuka
kuangalia picha za watu wanaokutana kimwili katika mitandao. Ni muhimu pia
kuepuka kusikiliza au kusoma habari za mambo machafu yanayohusu zinaa.
8. Ni muhimu kujihadhari na kuepuka watu wanaowasema wengine vibaya. Kwa kufanya hivyo utakuwa umejilinda na kuepuka kusengenya watu wengine. Na pia unakuwa umeepuka kusikiliza maneno ya usengenyaji. Kwa sababu hiyo utakuwa umeepuka kushiriki dhambi za wengine. "...wala usizishiriki dhambi za watu wengine". 1Timohteo 5:22.
9. Kuilinda imani yako. Unaweza kuilinda imani yako kwa
kuyakataa mafundisho ya uongo. Kamwe usikubali kuyafuata kwa sababu kwa
kufanya hivyo hautaurithi ufalme wa Mungu. Kwa mwamini aliyeokoka ili
aweze kufahamu mafundisho yaliyo ya kweli, na ni yapi yaliyo ya uongo, ni
muhimu kujifunza neno la Mungu kwa bidii na kulifahamu.
10.Kuishi maisha ya utakatifu.
Ni jambo la muhimu sana kwa kila mtu ambaye ameokoka
kufahamu ya kwamba ni lazima kuwa na utakatifu kama Mungu alivyo
mtakatifu. Maana yake ni kuishi maisha ya kumpendeza Mungu na kudumu katika
dhamiri safi. Mtu wa namna hiyo ni yule anayejilinda na kuepuka dhambi."Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi,
jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu
huyo aliku mkamilifu na uelekevu , ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na
uovu." Ayubu 1:1. "Twajua kuwa kila aliyezaliwa na Mungu
hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, na wala yule mwavu
hamgusi". 1Yohana
5:18. Kutokana na andiko hilo linaonyesha wazi
ya kwamba mtu ambaye amezaliwa (aliyeokoka) haiwezekani akafanya dhambi ikiwa
amejilinda na kuepukana na dhambi. Ikiwa mtu yeyote akisema hakuna
anayeweza kuwa mtakatifu kama Mungu au Yesu, huyo anapotea hayajui
maandiko ya neno la Mungu kwa ukamilifu. Maandiko yanashuhudia ya
kwamba mtu anaweza kuwa mtakatifu ikiwa anazitii sheria zote za Mungu.
Tunapoangalia kwenye Biblia katika Agano la kale na Jipya, maandiko
yamethibitisha ya kwamba walikuwepo watakatifu. Kwa sababu hiyo hata sasa
duniani wapo watakatifu ndio maana Mungu amesema; "Watakatifu waliopo duniani Ndio walio
bora, Hao ndio niliopendezwa nao". Zaburi 16:3.
11. Kuacha dhambi.
Ni muhimu kila mwamini aliyeokoka kufahamu ya kwamba ni jambo la
lazima kuacha kutenda dhambi. Ndio maana imeandikwa "Ikiwa mtu amekufa kwa mambo ya dhambi” na neno lingine linasema “usitende dhambi tena".
A. Kuhusu mtu kufa, hapa nitaelezea mambo yanayohusu dhambi.
Ikiwa mkristo aliyeokoka anampenda Mungu na kuishi neno la Mungu
linavyosema anakuwa amekufa kwa mambo ya dhambi. Dhambi haiwezi kumtawala tena,
na wala haina nafasi katika maisha yake. "...Tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa
mambo ya haki…" 1Petro 2:24.
B. Neno "Usitende dhambi tena" linamkataza mtu asirudie
kutenda dhambi. Kwa maneno mengine linamaanisha kuwa kamwe usitende dhambi na
pia kuziacha kabisa. "... Usitende dhambi tena, lisije likakupata
jambo lilo baya zaidi". Yohana 5:14.
12.Usiipende dunia na mambo yake na huku unamtumikia Mungu.
Hapa ninamaanisha ya kwamba mambo yale yote ambayo ni kinyume na
neno la Mungu ujitenge nayo na kuyaacha kabisa. Ni jambo la muhimu kujihadhari
na kuepuka kuishi maisha ya uvuguvugu katika kumtumikia Mungu kwa sababu
utakataliwa. Ikiwa mwamini anayo bidii katika mambo ya Mungu na huku
anaendelea na dhambi huyo ni vuguvugu. Mtu wa namna hiyo siku ile
ya mwisho atahukumiwa na kutupwa katika ziwa la moto ambalo ni Jehanum. Huko
atakuwa anateseka mchana na usiku yaani wakati wote, milele na milele. "Nayajua matendo yako, hu baridi
wala moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa
sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika
kinywa changu" Ufunuo 3:15-16; "Na moshi wa maumivu yao hupanda
juu hata milele na milele, wala hawana raha mchana wala usiku…" Ufunuo 14:11.
Maoni
Chapisha Maoni