Ni muhimu kwa kila mtu aliyeokoka kufahamu ya kwamba kanuni na utaratibu unaotakiwa kufuatwa wakati wa kuomba. Ndio maana Yesu alifundisha namna inayofaa kufuatwa na kufahamu wakati wa kuomba. Akasema “Tena msalipo, msiwe wanafiki, kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagagi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo ingia katika chumba cha ndani na ukiisha kufunga mlango wako, usalipo mbele ya Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke- payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua unayohitaji kabla ninyi hamjamwomba”. (Mathayo 6:5-7).Katika maandiko haya unaweza kuona namna Yesu alivyofundisha kwa kuwaonya wanafunzi wake.
Vilevile katika mafundisho hayo yanawahusu pia wale ambao wamekwisha kuokoka na kufanyika kuwa wanafunzi wa Yesu. Wakati wa kuomba inapasa mwamini kuepuka unafiki au kujionyesha ili kujulikana na watu wakati wa kuomba . Mafundisho haya yanahusu pia mambo ya maisha yetu mbalimbali. Kwa mfano, ikiwa mtu anataka kununua gari na moyoni mwake anataka kujionyesha mbele za watu ili ajulikane ya kwamba amenunua gari. Kwa kufanya hivyo atakuwa amejivuna na kujitukuza. Afanyaye hayo ni sawa na kutenda dhambi na ni machukizo mbele za Mungu. Kwa sababu hiyo Mungu hatayasikiliza maombi yake.
Neno kupayuka- payuka maana yake ni:
Kusema maneno yasiyofaa ambayo ni ya upumbavu na kupaza sauti kwa namna isiyofaa. Mfano ikiwa mtu yuko mbali na mwenzake na anamwita kwa kupaza sauti, kufanya hivyo ni njia mojawapo ya kupayuka.
Kutokana na mfano huo, kuna umuhimu wa kila mtu kuwa na busara wakati anapomwomba Mungu. Iwapo mtu yupo nyumbani kwake yampasa aombe bila kupayuka-payuka ili asiwasumbue wenzake (majirani).
Mtu binafsi anapofanya maombi ni muhimu kufanya maombi ya siri yeye na Mungu wake, si vyema kujulikana na kila mtu ya kwamba anamwomba Mungu.
Mfano mwingine ikiwa mtu wa Mungu ameenda hospitalini kuwaona wagonjwa na kufanya huduma ya kuwambea, aombe bila kupayuka. Kwa kufanya hivyo atakuwa amefanya maombi kwa busara bila kuwasumbua wagonjwa.
Kuhusu kuhubiri na kufundisha. Wakati wa kufanya mambo haya inapasa kufanya kwa umakini kwa ajili ya faida ya kanisa. Yapo mambo muhimu ya kuzingatia ambayo ni:
1.Anayehubiri au kufundisha ni muhimu kuhakikisha anafanya huduma kwa kuongea kwa sauti ya wastani ambayo itasikika vizuri kwa wanaomsikiliza yaani kanisa. Ikiwa sauti ni kubwa kupita kiasi inakuwa kelele na usumbufu kwa washirika. Na si hivyo tu hawawezi kusikia vizuri anachosema.
2. Jambo lingine la muhimu siyo vema kuweka kipasa sauti karibu sana na mdomo, kwa kufanya hivyo sauti itakuwa ya kukoroma na kutokusikika vizuri.
3. Kuhubiri na kufundisha kwa kusema haraka haraka, husababisha baadhi ya washirika kukosa kusikia vizuri na kuelewa. Kwa kufanya hivyo inakuwa ni sawa na kupayuka.
Maoni
Chapisha Maoni