Hapa tutajifunza na kufahamu kusudi la Mungu kwa watumishi wake
aliowachagua au kuwateuwa kwa ajili ya kazi yake. Katika somo hili tutajifunza
kusudi kuu ambalo Mungu amewaitia watumishi wake
ambalo ni KUHUBIRI
NA KUFUNDISHA neno lake. Hilo
ni jambo la msingi kwa ajili ya kuujenga ufalme wa Mungu. Ni muhimu kuwa makini
kuyathibitisha kwanza yale unayotaka kuhubiri au kufundisha, ili usije
ukalipotosha kanisa. Yatupasa kufahamu kwamba
wale tunaowafundisha ni watoto wa Mungu waliozaliwa katika Kristo Yesu wakati walipookoka. Kwa
sababu bado ni watoto wachanga hawayajui maandiko ipasavyo hivyo ni rahisi sana
kuamini kila kitu wanachofundishwa. Yakupasa mtumishi kujiuliza kuwa J e! yale
ambayo nimekua nikihubiri au kufundisha ni sahihi? Kama siyo sahihi yakupasa kulirekebisha kanisa kwa
kulifundisha upya ili kuliokoa
na jehanum ya moto wa milele. Kwa kufanya hivyo utakuwa ni mtumishi mwaminifu.
Kumbuka imeandikwa ya kwamba siku ile ya mwisho kila mmoja katika kazi ya
utumishi itapimwa mbele za Mungu na kutolewa hukumu.
Ndio maana Mtume Paulo
anaonya kwa kusema;
“Kwa kadri ya
neema ya Mungu niliyopewa, mimi, kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka
msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi
anavyojenga juu yake. Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka,
isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Kristo Yesu. Lakini kama mtu
akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au
majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri. Maana siku ile
itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu
kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Kazi ya mtu aliyeijenga juu yake ikikaa,
atapata thawabu.Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ila yeye mwenyewe
ataokolewa; lakini ni kama kwa moto.” 1Kor 2:10-15.
Ni jambo la kuvunja moyo kwa wale walioamini matangazo ya uponyaji wanapohudhuria kwenye mikutano ya injli wakitarajia kuponywa, lakini baadhi yao ni wachache tu ndio huponywa. Tukiangalia kwa upande wa kanisa neno la uponyaji linafundishwa ni haki ya kila mmoja aliyeokolewa na Bwana anapoliamini neno ataponywa. Ni vyema tukajifunza kwamba Mungu huponya na kufanya maajabu kwa ajili ya kusudi lake. Ndio maana andiko linasema; “Bwana amefanya kila kitu kwa kusudi lake...” Mit 16:4. Sehemu nyingine tunamwona Mtume Paulo sio wote aliwaponya wakati wa utumishi wake. Ndio maana alisema “...Trofimo nalimwacha huko Mileto, hawezi”. 2Tim 4:20b
Kuna mambo anayotakiwa mtumishi kuyazingatia
ili aweze kulifahamu zaidi neno la Mungu. Ni haya yafuatayo;
1. Kujifunza neno la Mungu kwa bidii kwa kulisoma na kulielewa
2. Kujifunza kwa kuwasikiliza watumishi wengine wanapofundisha.
3. Kujfunza kwa kusoma vitabu vya watumishi wengine.
1. Kujifunza neno la Mungu kwa bidii kwa kulisoma na kulielewa
2. Kujifunza kwa kuwasikiliza watumishi wengine wanapofundisha.
3. Kujfunza kwa kusoma vitabu vya watumishi wengine.
Ni muhimu kwa kila mafundisho ya
neno la Mungu kuyachambua na kuyathibitisha na maandiko ili kufahamu ukweli
kama ndivyo ulivyo. Kutokujua kanuni hizi ni rahisi kuamini kila
kinachofundishwa ambacho mwisho wake ni njia ya upotevu.
Kwa mfano huwezi kutafsiri andiko
katika mstari mmoja na kuusimamia peke yake. Ili kupata uthibitisho ni lazima
ulinganishe na maandiko mengine katika Biblia. Tunaweza kujifunza kwa wakati
ule wa mitume jinsi watu wa Beroya walivyokuwa na bidii ya kuyachunguza maandiko.
“Mara hao ndungu
wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya...Watu hawa walikuwa waungwana
kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa
walilipokea, lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku,
waone mambo hayo ndivyo yalivyo.”
Mdo 17:11.
Ikiwa utajihesabia haki yakwamba
unayajua maandiko kuliko wengine na kupuuza kujifunza kutoka kwa wengine,
kufanya hivyo ni kujidanganya nafsi yako mwenyewe. Ni jambo la msingi kuendelea
kujifunza neno kwa wengine, kwa sababu kila mmoja amepewa ufunuo wa neno la Mungu
kwa sehemu, kwa ajili ya kujengana kila mmoja na mwenzake. Ijapokuwa kuna
watumishi ambao wamejaliwa kuyafahamu maandiko kwa usahihi na kuyahubiri na
kuyafundisha, lakini kuna kitu ambacho watakuwa wamepungukiwa watajifunza kutoka
kwa wengine. Ndio maana imeandikwa; “Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na kufanya unabii kwa
sehemu...wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajaua sana kama mimi
nami ninavyojuliwa sana.” 1Kor 13:9,12. “Tena pana tofauti
za huduma na Bwana ni yeye yule. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa roho kwa
kufaidiana (kusaidiana au kujengana) .”1Kor 12:5,7. “Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadri ya kipimo cha
kipawa chake Kristo.” Efe 4:7.
Kama ambavyo umeona mwanzoni, nimezungumzia
kusudi kuu la Mungu kwa watumishi wake aliowaita kuhubiri na kufundisha neno la Mungu. Je!
Watahubiri na kufundisha nini? Fuatana na nami na kuangalia haya
yafuatayo;
1. Kuwahubiria watu wenye
dhambi watubu na kuziacha dhambi zao. Jambo hili tunajifunza kwa Yesu Kristo Bwana
wetu na kwa mitume wake. “Tokea wakati huo
Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni, kwa maana ufalme wa Mungu
umekaribia.” Mt 4:17. “Tubuni, basi,
mrejee, ili dhambi zenu zifutwe...” Mdo 3:19.
2. Kuwafundisha
neno la Mungu wale ambao wamekwisha kumwamini Yesu na kuokoka. “Yesu akaja kwao,
akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi,
enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi,...na kuwafundisha kuyashika
yote niliyowamuru ninyi...” Mt 28:18-20.
Kutokana na kusudi kuu ambalo
umejifunza ni vyema kuwa na kiasi katika kuhubiri au kufundisha mambo haya
yafuatayo;
1. Uponyaji na miujiza. Hapa ninatoa mfano ikiwa mtumishi wa Mungu wakati
ameandaa mkutano wa injili kwa kuwatangazia watu kuwa mkutano utafanyika mahali
fulani. Siyo sahihi anapowawakaribisha watu ili kusikiliza habari njema na kuwaambia
njoo upokee muujiza wako na wenye shida na
magonjwa wataombewa na kuponywa. Lakini jambo la msingi na la kuzingatia ni
kuhubiri na kufundisha neno, naye Mungu atajidhihirisha kwa ishara na maajabu
kwa ajili ya kulithibitisha neno (fundisho).
Tuangalie mitume wa Yesu kama
ilivyoandikwa; “Nao
wale wakatoka (mitume) ,wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na
kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.” Mk 16:20.
Ni muhimu kutambua kwamba sisi tu wanadamu
hatuna uwezo wa kuponya bali tunapewa uwezo wa kuponya na Mungu mwenyewe.
Hapa ina maana kwamba uwezo wa kuponya
si mali yetu na kuutumia kama tupendavyo, bali ni Bwana huwatumia watumishi
wake kama apendavyo. Kwa maana hiyo watumishi walioitwa kuifanya kazi ya Bwana
wao ni kama chombo ambacho hutumiwa na Bwana.
Ni jambo la kuvunja moyo kwa wale walioamini matangazo ya uponyaji wanapohudhuria kwenye mikutano ya injli wakitarajia kuponywa, lakini baadhi yao ni wachache tu ndio huponywa. Tukiangalia kwa upande wa kanisa neno la uponyaji linafundishwa ni haki ya kila mmoja aliyeokolewa na Bwana anapoliamini neno ataponywa. Ni vyema tukajifunza kwamba Mungu huponya na kufanya maajabu kwa ajili ya kusudi lake. Ndio maana andiko linasema; “Bwana amefanya kila kitu kwa kusudi lake...” Mit 16:4. Sehemu nyingine tunamwona Mtume Paulo sio wote aliwaponya wakati wa utumishi wake. Ndio maana alisema “...Trofimo nalimwacha huko Mileto, hawezi”. 2Tim 4:20b
Yatupasa tujihadhari tusiwahukumu
wale ambao hawajaponywa na kudhani ni kwa sababu hawaamini au ni wenye dhambi. Kuna wakati Yesu alikwenda kwenye birika liitwalo Bethzatha
ambapo palikuwa na jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete,
nao waliopooza. Ijapokuwa aliwakuta wagojwa wengi kwenye hilo birika,
hapo Yesu alimponya mtu mmoja. Soma kwenye Yn 5:1-9. Sehemu nyingine alipokwenda aliwaponya wagonjwa wote. “Wakamwendea makutano mengi wakimletea viwete,
vipofu, mabubu, vilema, na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; akawaponya.”
Mt 15:30. Pia unaweza kujifunza wakati
Yohana mbatizaji alipokuwa gerezani Yesu
alikuwa anafufua wafu. Lakini Yohana alipouawa Yesu hakumfufua.
Kuna kisa cha mtumishi mmoja na
mke wake, mtoto wao aliumwa wakamwombea ijapokuwa hali yake ilizidi kuwa mbaya
waliendelea kusimamia imani na kumwamini Mungu kuwa atamponya, lakini mtoto alikufa. Pia kuna kisa
kingine cha mwinjilisti mmoja ambaye Bwana alikuwa anamtumia kuponya wagonjwa. Siku
moja alimkuta mtu aliyekuwa mgonjwa alifikiri atakapomwombea Bwana ataponya
kama alivyomtumia kuponya wengine, lakini alipomwombea yule mtu hakuponywa. Kama yule mgonjwa asingewahishwa
hosipitali angekufa.Ikiwa mtu mgonjwa
anapoombewa hupona wakati huo huo, kama hajaponywa apelekwe hospitali.
2 .Utajiri au mafanikio. Hili ni jambo lingine ambalo linahubiriwa au
kufundishwa kinyume na neno la Mungu. Ni muhimu kuwa makini kuliangalia neno na
kulitumia kupima kila kitu tunachokifanya kama ndivyo kinavyotakiwa. Neno la Mungu ni kiongozi, linatuongoza kwa
kila jambo katika maisha ya hapa duniani. Vilevile neno la Mungu linatufundisha na
kutuweka huru kwa yale tusioyafahamu. Ndiyo
maana imeandikwa; “Tena mtaifahamu kweli,
nayo hiyo kweli itawaweka huru.”
Yn 8:32.
Mungu amesema masikini wataendele
kuwepo hapa duniani. “Kwa maana masikini hawatakoma katika nchi milele,...”
Kum 15:11.
Kwa hiyo siyo sahihi
kuwahubiria watu ya kwamba Mungu
atawafana matajiri ikiwa watamtolea Mungu fungu la kumi, sadaka, au wakitoa
michango kwa ajili ya kupeleka injili. Kumtolea Mungu zaka na dhabihu ni sehemu
na ni agizo la kumwabudu kwa kumrudishia
utukufu kwa yale aliyokupa au aliyokufanikisha. Kwa kutii na kufanya hivyo tayari utakuwa umebarikiwa. Kubarikiwa
kwa mtu si kwa wingi wa fedha na mali alizonazo pekee, bali ni kwa kuishi
sawasawa na neno la Mungu.
Katika maandiko tunajifunza jinsi Yesu alivyoacha enzi na mamlaka ya mbinguni, utajiri na uungu aliokuwa nao, akaja
duniani kama mtumwa. Kwa sababu hiyo hakuwa tajiri. Naye mama yake Yesu alikuwa
ni mtu wa kawaida wala si tajiri. Lakini walikuwa ni wabarikiwa. “Na abarikiwe yeye
ajaye kwa jina la Bwana...” Zab
118:26. “Nayo
siku y pili yake watu wengi walioijia sikukuu walisikia Yesu anakuja
Yerusalemu...wakatoka nje kwenda kumlaki, wakapiga kelele, Hosana! Ndiye
mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana, Mfalme wa Israel.” Yn 12:12-13. “Basi, Mariamu
akaondoka siku hizo, akaenda...nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti. Ikawa
Elisabeti aliposikia kuamkia kwake...akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa
nguvu akasema, umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako
amebarikiwa.” Lk 1: 39-42.
Injili inayohubiriwa ya mafanikio
imewayumbisha watu wengi kwa sababu walitarajia watakuwa na yale yote
walioamini na kuombewa. Ni vema tujiulize je! Watu wote waweza kuwa matajiri?
Jibu ni hapana kwa sababu Mungu anamngawia kila mtu kipimo au kiasi cha Baraka (mafanikio) “...Kutoa
sadaka ya hiari ya mkono wako, utakayoyatoa kwa kadiri akubarikiavyo Bwana Mungu wako.
Kila mtu atoe kwa kadiri awezavyo, kwa
kadiri ya baraka ya Bwana, Mungu wako alivyokupa. ” Kum 16:10,17.
Kutokana na somo hili la utajiri
au mafanikio tunaona na kufahamu ya kwamba Mungu anawabarikia watu wake kwa
kipimo. Ndiyo maana Mungu amesema kila mtu atoe sadaka kwa kadiri alivyombariki.
Maoni
Chapisha Maoni