Chanzo cha imani
“Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la
Kristo” Rum 10:17. Imani inatokana na neno la Kristo au neno
la Mungu, mtu akilisikia neno na kulifahamu na kuliamini anakuwa na imani
katika neno la Mungu. Ni jambo la msingi na muhimu kuliamini neno, ndio maana
Mungu amesema; "Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa
imani; Naye akisita-sita; roho yangu haina furaha naye” Ebr 10:38.
Kuamini neno la Mungu.
Asiyeamini neno la Mungu hampendezi Mungu bali amemwasi, hataingia
mbinguni. Wana wa Israel walikufa jangwani kwa sababu hawakuamini maneno ambayo
Mungu aliowaambia. “Tena ni akina nani aliochukizwa nao miaka
arobaini? Si wale waliokosa, ambao mizoga yao ilianguka jangwani? Tena ni akina
nani aliowaapia ya kwamba hawataingia katika raha yake (mbinguni), ila wale walioasi? Basi twaona ya kuwa
hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutoamini kwao. Maana ni kweli, sisi nasi
tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lilosikiwa
halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanganyika na imani ndani yao waliolisikia” Ebr 3:17-19; 4:2.
Imani na matendo.
Mtu anawezaje kuwa na imani na matendo? Anapoliamini neno na
kuishi linavyosema, imani ya mtu huyo ni hai. Imani bila matenda haifai
imekufa, bali inakamilishwa na matendo.“Vivyo hivyo na imani, ispokuwa na matendo, imekufa nafsini mwake.
Lakini mtu atasema, wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako
pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu. Waona
kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile
ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale. Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa
na haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake” Yak 2:17,18,22,24.
Kumtumaini Mungu kwa imani.
Mungu yeye ni mkuu wa yote na ni muumbaji wa yote, anatawala
duniani na mbinguni na katika yote. Yeye anaweza yote, na amwaminiye yote
yawezekana kwake. Mwanadamu anapaswa kumtumaini na kumkiri katika mambo
yote na njia zote naye atamfanikisha. Ili Mungu amfanikishe ni lazima aishi kwa
kuyafanya maagizo ya neno lake. “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala
usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye
atayanyosha mapito yako” Mit 3:5,6.
“Umtumaini Bwana ukatende mema (maagizo yake), Ukae katika inchi , upendezwe na uaminifu,
Nawe utajifurahisha kwa Bwana, Naye atakupa haja za moyo wako. Umkabidhi Bwana
njia yako, Pia umtumaini, naye atafanya”Zab37:3-5. “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule
amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, Na moyoni mwake
amemwacha Bwana. Amebarikiwa mtu yule amtegemeaye Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini
lake” Yer17:5,7.
Kusema kwa imani.
Ili uweze kusema kwa imani na mambo yatokee, yapo mambo ambayo
unapaswa kuyafahamu.
1.Umtumaini
na kumwamini Mungu, hii ni imani ya Kimungu. Ndio
maana Bwana wetu Yesu Kristo alisema “mwaminini Mungu” hili neno lina maana ya kuwa na imani ya
Kimungu.“Yesu akajibu,
akamwambia, mwaminini Mungu” Mk 11:22.
2. Kuishi sawa swa na neno la Mungu. Imeandikwa, Mungu anafanya kazi na wale
wampendao ni wale wanaolishika neno lake. “Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda,
atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya
makao kwake” Yn 14:23. “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote
Mungu hufanya kazi na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani,wale
walioitwa kwa kusudi lake” Rum 8:28.
3. Kudumu katika maombi na wakati mwingine
kufunga. Bila
hivyo huwezi kufanya mambo ya mamlaka katika Mungu, iwe
kuhamisha mlima au kutoa pepo. “……Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima
huu, ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno
lisilowezekana kwenu. [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na
kufunga.]” Mt 17:20,21. Katika maandiko haya Yesu anatufundisha
yote yawezekana kwa imani kidogo, ikiwa tunaomba na kufunga.
Maoni
Chapisha Maoni