Neno MAOMBI linamaanisha kupeleka
hitaji/mahitaji mbele za Mungu kwa ajili ya kupatiwa msaada.
Unapomwomba Mungu kitu chochote ni muhimu ujue anakusikia. Ni sawa na mtoto
anapomwomba baba yake kalamu au daftari anamsikia na kumpa.Unapomuomba Mungu
unaongea na Baba yako wa mbinguni naye anakusikia kama baba wa dunia hii
anavyomsikiliza mtoto wake. “Au kuna mtu yupi
kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa
nyoka? Basi ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! si
zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema (mahitaji) wao wamwombao”? Mathayo 7:9-11.
Jinsi ya kuomba
1. Kuomba kwa imani.
Ili uombe kwa imani ni lazima uwe na imani, na imani inapatikana
katika neno la Mungu. “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na
kusikia huja neno la Kristo” Warumi 10:17. Unapomwomba Mungu ni lazima uamini
kile kitu ambacho umemwomba amekupa, bila ya kuwa na shaka yoyote nawe
utapokea. “Amin, nawaambia, ye yote atakayeuambia
mlima huu, ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini
kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, yo
yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapoke, nayo yatakuwa yenu” Marko 11:23, 24.
“Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo
yatarajiwayo, ni bayana (wazi) ya mambo yasiyoonekana. Lakini pasipo
imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini
kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao” Waebrania 11:1,6. “Na kama tukijua kwamba atusikia,
tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba” 1Yohana 4:15.
2. Kuomba katika utakatifu
Ili uombe katika utakatifu yakupasa kuishi maisha ya utakatifu,
haya ni maisha ya haki. “Bwana yu mbali na wasio haki; Bali
huisikia sala ya mweye haki” Mithali 15:29. “Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye
dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo” Yohana 9:31. “Wapenzi mioyo yetu isipotuhukumu,
tuna ujasiri kwa Mungu; na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa
twazishika amri zake,na kuyatenda yapendezayo machoni pake” 1Yohana 3:21,22.
3. Kuomba katika Roho Mtakatifu
Mtu ili aombe katika Roho Mtakatifu ni muhimu awe amejazwa Roho
Mtakatifu kama wale Mitume wa Yesu. “Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza
kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka” Matendo 1:4. “Bali, ninyi wapenzi, mkijijenga juu ya
imani… takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu” Yuda 1:20.
“Kwa sala zote na maombi mkisali
kila wakati katika Roho”...Waefeso 6:18. Yesu Kristo alishukuru katika Roho
Mtakatifu, “Saa ile ile alishangilia kwa Roho
Mtakatifu, akasema,Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo
haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam,
Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza” Luka 10:21.
4. Kuomba
katika mapenzi ya Mungu
Ni kuomba sawa sawa na neno au maagizo ya Mungu na wala si
vinginevyo. Kwa mfano huwezi kumuomba Mungu akusaidie na kukufanikisha kufanya
uovu wowote kama ujambazi, namna hii ni kuomba vibaya, Mungu hasikii maombi
kama haya. Ni muhimu uyafahamu maandiko yote ya neno la Mungu usije
ukaomba vibaya. “Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya
kuwa, tukiomba kitu sawa sawa na mapenzi yake, atusikia” 1Yohana 5:14. “Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu
mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tama zenu” Yakobo 4:3.
Maoni
Chapisha Maoni