Mungu alituumba kwa kusudi la kuishi katika maadili ya neno lake,
ndio maana imeandikwa, “Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika
Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili
tuenende nayo” Waefeso 2:10.
Mavazi ya mwanamke
Neno lake Mungu linatufundisha maadili ya mavazi ya kuvaa kwa
mwanamke. Vivyo hivyo wanawake wajipambe kwa
mavazi ya kujisitiri…" 1Timotheo 2:9. Ikiwa mwanamke amevaa gauni fupi,
linalobana au lililopasuli na kuonyesha sehemu zake za mwili ambazo hazipaswi
kuonekana wazi anajiabisha na kujivunjia heshima mbele za Mungu na jamii.
Kujichubua uso ni kuondoa rangi ya asili aliyoumbwa nayo. Kunyoa nyusi na
kupaka rangi badala ya
nyusi na kuvaa nywele badia, haya si maadili ya neno la Mungu.
Mwanamke afanyaye mambo kama haya hapa juu anampinga
na kumkosoa muumbaji wake ambaye ni Mungu. Ni sawa na kumwambia
alikosea alivyomuumba. Si vema kumkosoa Muumbaji wake kwa matendo hayo. Yeye ni
mkuu, hakosei ni mwenye haki wakati wote.“Ole wake ashindanaye na Muumba wake!
Kigae kimoja katika vigae vya dunia! Je! Udongo umwambie yeye afinyangaye;
Unafanya nini? Au kazi yako, Hana mikono? Mimi nimeumba dunia, nimemhuluku
mwanadamu juu yake; Mimi, naam, mikono yangu mimi, imezitandaza mbingu, na
jeshi lake lote nimeliamuru” ISaya 45:9,12. Hatuwezi kumfundisha wala kuhoji uumbaji
wake kwa sababu imeandikwa, “Mungu akaona kila kitu alichokifanya na
tazama ni chema sana…” Mwanzo 1:31.
Kuvaa mavazi ya namna hiyo ni kuharibu watoto ambao ni taifa la
wakati ujao. Watoto hujifunza kwetu kwa yale wanayoyaona tunafanya yawe ni mabaya au ni
mema. Kwa hiyo wazazi wanapaswa kuvaa mavazi ya heshima na kusitiri mwili ili
kuficha maeneo yote ya mwili yasiyopaswa kuonekana. Kwa mfano huwezi kusema
Mungu anaangali mambo ya rohoni na kwamba haangalii mambo ya mavazi. Si vyema
kusema hivyo kwa kuwa Yesu aliwafundisha waandishi na Mafarisayo, wanapaswa
kusafisha kikombe ndani na nje ili kiwe safi.
Katika maneno hayo Yesu alimaanisha ya kwamba haiwezekani kuwa
safi kwa nje na ndani ni kuchafu, bali nje na ndani kunapaswa kuwa safi. “Ole wenu waandishi na Mafarisayo,
wanafiki! Kwa kuwa mwasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa
unyang’anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya
kikobe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi” Mathayo 23:25,26.
Mavazi ya mwanamume
Pia mwanamume anapaswa kuvaa mavazi ya heshima na kusitiri mwili ,
haya ndio maadili ya neno la Mungu. Hapaswi kuiga namna ya dunia hii na kuvaa
mavazi kwa namna isivyo sahihi, kama kufungia suruali katikati ya makalio
(mlegezo) na kuacha kifua wazi, mambo haya hayapendezi mbele za Mungu. “Basi ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma
zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu; ndiyo ibada yenu yenye maana.
Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mngeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu,
mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kupendeza, na ukamilivu” Warumi 12:1,2.
Kuimba mbele za Mungu.
Tunapokuwa tunafanya ibada mbele za Mungu iwe ni kusifu, kuabudu, kuimba na
kucheza inatupasa kujua tuko mbele ya Mungu mkuu anayestahili kuhofiwa na
kuheshiwa na wanadamu wote. “Nchi yote na imwogope Bwana,Wote wakaao
duniani na wamche” (kumhofu) Zaburi 33:8. Mungu hafanyiwi dhihaka ya kuchezewa
sawa na mtoto anavyoweza kuchezea mwana sesere kama apendavyo. Vile vile hatuwezi
kumfurahisha Mungu wetu kwa kuimba na kucheza kwa namna ya dunia hii.
Hayo hayampendezi Mungu na kwa neno lake anasema hivi, “Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa
maana sitaki kuzisikia sauti za vinanda vyenu. Lakini hukumu na itelemke kama maji,
na haki kama maji makuu” Amosi 5:23,24. Ni vema wewe uliyekwisha kumjua Mungu
yakupasa kufanya ibada ya kumpendeza mbele zake. Ametupa maadili ya neno lake kuhusu jinsi ya kufanya ibada ya
kupendeza kwa kuimba na kucheza kwa namna nzuri. Imeandikwa, “Mwabuduni Bwana kwa uzuri na utakatifu,
Tetemekeni mbele zake, nchi yote” Zaburi 96:9.
Kwa mfano, kufanya mikutano ya injili kwa kuimba na kucheza kwa
mapigo na sauti ya miziki ya namna ya dunia ili watu wasioamini wavutiwe na kuokoka. Kwa kufanya hivyo si sahihi ni
kulitukanisha jina la Bwana kana kwamba hana nguvu na uwezo wa kuokoa watu
wake, hili nalo ni dhambi, kama
hutatubu na kuacha kufanya hivyo utahukumiwa. “Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala
hayatendi, kwake huyo ni dhambi” Yakobo 4:17. Mungu ndiye anayeokoa watu kwa neno lake
si mwanadamu kwa kuwavuta kwa kuimba na kucheza miziki ya kidunia. Yesu alisema;
Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho. Yohana 6:44
Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho. Yohana 6:44
Kuimba na kucheza
Kuimba na kucheza inakubalika mbele za Mungu kwa kutumia vyombo. “Msifuni kwa mvumo wa baragumu; Msifuni
kwa kinada na kinubi; Msifuni kwa matari na kucheza; Msifuni kwa zeze na
filimbi; Msifuni kwa matoazi yavumayo sana. Kila mwenye punzi na amsifu Bwana.
Haleluya” Zaburi 150:3-6.
Maoni
Chapisha Maoni