Tunda hili linadhihirisha upendo wa Mungu kwa wanadamu ijapokuwa ni wenye dhambi ambao hawastahili mbele zake. Mungu ni wa kwanza kutupenda kwa sababu andiko linasema, “....Yeye alitupenda sisi kwanza. 1Yoh 4:19". Ndio maana alimtoa mwanawe Yesu Kristo aje hapa duniani ili kupitia yeye kila mtu aokolewe na kuwa na uzima wa milele. Ndio maana imeandikwa, “....Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye Yn 3:16-17."
Kwa upendo wake Mungu alitupenda bure, na kwa neema yake akamtuma Mwanawe Yesu Kristo aje kutupatanisha na Mungu. Ndio maana andiko linathibitisha kwa kusema, “Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu 1Yoh 4:10." Kwa sababu Mungu alitupenda yatupasa sisi kumpenda kama andiko linavyosema, “Wapenzi, ikiwa Mungu alitupenda hivi, imetupasa na sisi kupendana. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote. Tukipendana Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilishwa ndani yetu....Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake. 1Yoh 4:11-12, 16."
Mambo ya kuzingatia na kuishi katika pendo Mungu. Ni haya ifuatavyo:
1. Kuzitii sheria za Mungu.
“Katika hili twajua kwamba twawapenda watoto wa Mungu , tumpendapo Mungu, na kuzishika amri zake.” 1Yoh 5:2. Anayeishi katika pendo siku ile ya mwisho hatahukumiwa. “Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu; kwa kuwa, kama yeye alivyo, ndivyo na sisi tulivyo ulimwenguni humu, Katika pendo hamna hofu ; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu, na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo.” 1Yoh 4:17-18.
2. Kupendana kila mtu na mwenzake. Haiwezekani kumpenda Mungu bila sisi kupendana. Ndio maana imeandikwa, “Mtu akisema, nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake,ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake.” 1Yoh 4:20-21.
3. Kuwapenda adui zetu na wale wanaotuudhi. Kwa kuwa Yesu alinasema, “....Wapendeni adui zenu waombeeni wanaowaudhi; ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni....Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu. Mt 5:44-45,48."
4. Kuepuka kuipenda dunia na mambo yake.
Kuipenda dunia na mambo yake ni pale mtu anapokuwa na tamaa mbaya. Kwa hiyo mtu aliye na tamaa mbaya kila kitu anacho kiona anataka awe nacho. Kwa mfano ameona toleo jipya la simu, viatu, nguo, au kitu kingine chochote anakitamani. Jambo la msingi hapa yampasa mtu kupanga na kuzingatia yale mahitaji ya muhimu katika maisha. Imeandikwa “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichopo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.” 1Yoh 2:15-17."
"1 Timotheo 6
6 Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa.
7 Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu;
8 ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo.
9 Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu.
10 Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi."
Kutokana na maandiko hayo yanatufundisha jinsi ya kuepuka tamaa mbaya, ni pale tunaporidhika kwa yale mahitaji yote ya muhimu katika maisha yetu. Kwa sababu hiyo tunakuwa na kiasi katika maisha yatu.
Maoni
Chapisha Maoni